Quotessence
Home / Books / Kolonia Santita

Kolonia Santita

Book by Enock Maregesi · 13 quotes · John Murphy, John Murphy Ambilikile, Murphy

Filter quotes by topic

Kolonia Santita Quotes

“Lakini, akiendelea kuwaza na kuangaza, ghafla Murphy aliona kitu kama gari likiwa limesimama kwa mbali. Alisimama na kupata hamu ya kujua. Murphy alianza tena kutembea, lakini sasa akiifuata ile gari, halafu akaongeza mwendo na kukimbia; macho yote yakiwa mbele! Alipofika, karibu na gari ile, hakuminya kifyatulio kumpiga mtu risasi. Alijenga tabasamu na kuongeza mwendo. Gari ilikuwa Ferrari Testarrosa ya Lisa Madrazo Graciano!”

“Nusu dakika baada ya kuondoa gari, Murphy aliona kiwiliwili cha mtu kikimwendea mbio kutokea katika nyumba ya magaidi! Hapohapo alisimamisha gari na kuacha taa zikiwaka, halafu akashika bunduki na kushuka – akiwa ameangalia mbele kwa tahadhari kubwa. Alikuwa mwanamke. Debbie! Murphy alipojua ni Debbie, alitupa bunduki na kuchomoka mbio mpaka wakakutana na kukumbatiana kwa nguvu! Murphy alimbeba Debbie na kumbusu kila sehemu, halafu akamfuta machozi na kumbembeleza.”

“Lakini kabla Rais hajaendelea kuongea, na ‘John Murphy wa Kolonia Santita’, Mogens aliruka na kumnyang’anya simu. “Ambilikile,” Mogens aliita, akiangalia saa. “Brodersen,” Sauti ya upande wa pili ilijibu, baada ya sekunde kumi. “60111906,” Mogens alisema, baada ya sekunde kumi. “57121906,” Sauti ya upande wa pili ikajibu, baada ya sekunde kumi. “Jumapili,” Mogens aliendelea, baada ya sekunde kumi. “Ijumaa,” Sauti ya upande wa pili ikajibu, baada ya sekunde kumi. John Murphy wa Kolonia Santita aliposema ‘Ijumaa’, Mogens aliunda kicheko na kurusha mkono katika matundu ya kuongelea ya simu ...”

“Peter, naomba nitubu kosa. Mimi si mtoto wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Ni mtoto wa Rais wa Meksiko. Lisa ni mtoto wa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” Debbie alisema akitabasamu. “Hata mimi nilijua ulikuwa ukinidanganya. Lakini mbona Rais wa Meksiko haitwi Patrocinio Abrego?” Murphy aliuliza. “Utamaduni wa Meksiko ni tofauti kidogo na tamaduni zingine,” Debbie alijibu baada ya kurusha nywele nyuma kuona vizuri. “Hapa, watu wengi hawatumii majina ya pili ya baba zao. Hutumia jina la kwanza la mama la pili la baba; ndiyo maana Wameksiko wengi wana majina matatu. Kwa upande wangu, Patrocinio ni jina la baba yake mama yangu na Abrego ni jina la babu yake mama yangu – kwa sababu za kiusalama.”

“Murphy hakupenda kupoteza muda. Alinyanyuka na kumimina risasi, Mungu akamsaidia akadondosha wawili huku wengine wakipotea kwa kuruka vibaya na kukwepa. Kwa kasi Murphy alikimbia huku ameinama mpaka katika milango mikubwa ya nje, ambayo sasa ilikuwa wazi. Hapo akasita. Chochote kingeweza kumpata kwa nje kama hangekuwa mwangalifu. Bunduki yake ilishakwisha risasi. Aliitupa na kuchungulia nje akaona adui mmoja akikatisha kwenda nyuma ambako ndiko mashambulizi yalikokuwa yakisikika sasa. Murphy hakumtaka huyo. Aligeukia ndani kuona kama kulikuwa na bunduki aichukue lakini hata kisu hakikuwepo. Akiwa bado anashangaa, ghafla alitokea adui – kwa ndani – na kurusha risasi, bahati nzuri akamkosa Murphy. Murphy, kama mbayuwayu, aliruka na kusafiri hewani hapohapo akadondoka nyuma ya tangi la gesi karibu na milango ya nje. Alipoona vile, adui alidhani Murphy alidondoka mbali. Alibung’aa asijue la kufanya. Wasiwasi ulipomzidi alishindwa kuvumilia. Alishika bunduki kwa nguvu na kupiga kelele, "Yuko hukuuu!" Halafu akajificha ili Murphy asimwone. Lakini Murphy alikuwa akimwona.”

“Usiwe na wasiwasi, Peter. Hizo ni hisia zangu tu. Huwezi kuwa mpelelezi. Lakini, kusema ule ukweli, ningependa sana kuonana na John Murphy. Kuna kazi binafsi ningependa kumpa. Wewe unatoka Afrika, hujawahi kumwona?” Debbie alizidi kumshtua Murphy. “Nani?” Murphy aliuliza huku akitabasamu. “John Murphy wa Afrika.” “Sijawahi kumwona. Mbona unamuulizia hivyo?” Debbie alitulia. Kisha akarusha nywele ili aone vizuri. “Nampenda sana!” “Kwa nini?” “Simpendi kwa mahaba, lakini.” “Ndiyo. Kwa nini?” “OK. Nampenda kwa kipaji chake. Alichopewa na Mungu, cha ujasusi. Kusaidia watu.” “Ahaa!” Murphy alidakia, sasa akifikiri sana. “Murphy ana mashabiki wengi hapa Meksiko bila yeye mwenyewe kujua, kwa sababu ya kupambana na wahalifu wa madawa ya kulevya – hasa wa huku Latino. Tatizo lake haonekani. Wengi hudhani ni hadithi tu, kwamba hakuna mtu kama huyo hapa duniani.” “Hapana! Murphy yupo! Ni mfanyabiashara maarufu huko Tanzania. Lakini ndiyo hivyo kama unavyosema ... Haonekani!”

“Murphy. Sina mbinu zozote za kujikinga kama unavyojua; mbali na mafunzo ya FBI. Baada ya kumrusha nyoka wa Lisa nywele zilinisisimka. Wazo la kukimbia likaja ghafla. Kukimbia hata hivyo nikashindwa kwa kuhofu huenda wangeniona. Hivyo, nikarudi nyuma ya nyumba na kupanda mti na kujificha huko. Bunduki zilipolia, nilijua wamekuua. Ila kitu kimoja kikanishangaza: mashambulizi hayakuonekana kukoma. Kitu hicho kikanipa nguvu kwamba huenda hujafa na ulikuwa ukipambana nao. Kimya kilipotokea nilijua umewashinda nguvu, kitu ambacho kumbe kilikuwa kweli. Nilipokutafuta baadaye lakini bila kukuona kutokana na kukurukakara za maadui niliamua kwenda katika gari ili nije na gari kama mgeni, nikitegemea waniruhusu kuingia ili nipate hakika kama wamekuua au bado uko hai. Wasingenifanya chochote. Kimaajabu, niliposhuka katika mti ili nikimbie katika gari, niliona gari ikija kwa kasi. Kuangalia vizuri nikakuta ni Ferrari, halafu nikashangaa nani anaendesha gari ya Lisa!” Murphy alitabasamu tena na kuendelea kusikiliza. “Sijui moyo wangu ulikuwaje. Sikuogopa tena! Badala yake nilikaza mwendo na kuendelea kuifuata huku nikipata wazo hapohapo kwamba mtu aliyekuwemo akiendesha hakuwa adui. Adui angeingia katika gari na kunisubiri aniteke nyara.” Debbie alitulia. “Ulihisi ni mimi?” Murphy aliuliza. “Nilihisi ni mtu tu mwema amekuja kunisaidia ... au mwizi wa gari. Hata hivyo, baadaye nilijua ni wewe na furaha yangu yote ilirudi.”

“Ndani ya chumba, akiwa bado amechanganyikiwa, akiwa hajui Debbie alikokwenda, Murphy alisikia walinzi wakipiga kelele nje. Kamanda huwa anakuwa shetani nyakati kama hizo. Alibeba pumzi. Mikononi mwake akiwa na M-16, Debbie kichwani; Murphy alishangaza umati wa watu! Risasi zaidi ya sitini zilifyatuka katika bunduki, mlango wote ukabomoka – ndani ya sekunde kumi!”

“Ngumi ya Ambilikile ilitua barabara katika kichwa cha Brookshield na kuleta madhara makubwa. Sehemu moja ya kichwa, cha Brookshield, ilibonyea kabisa! Kimya kilichotawala kiliwasisimua mashabiki. Walipovamia ulingo, kushuhudia kisichoweza kufikirika, walitoka pale wakiwa na hakika ya asilimia 100; kwamba John alikuwa na nyundo (au chuma chochote) katika mfuko wake wa bukta – aliyoitoa (harakaharaka), wakidhani ni mtindo wa kipigo, na kumpondea mwenzake kichwani! Ile haikuwa nyundo. Wala haukuwa uchawi. Ilikuwa ngumi, imara, ya uzito wa kilo 90; uzito wote wa John Ambilikile.”

“Vijana wa Tume walipofika kambini chini ya ulinzi mkali wakiwa na Kahima, polisi wengi walionekana kuwapigia saluti lakini wakubwa wao wakawakataza na kuwambia wao walikuwa watu wa kawaida kama wao. Walisindikizwa na lundo la polisi mpaka ndani ya jumba la utawala Murphy alimokuwa ameuhifadhi mwili wa Radia. Walipofika walishtuka, na hata kuwashangaza polisi. Mwili wa Radia haukuwepo! Walitafuta kila sehemu, na kuwambia polisi wawasaidie kutafuta, lakini Radia alishapotea. Murphy alipata wazo na kutoka nje, kwa kukimbia, polisi wengi wakimfuata; mpaka katika helikopta ya DEA ambapo alifungua mlango na kuingia ndani. Ndani ya helikopta hakukuwa na mtu!”

“Radia Hosni alikuwa na bahati kuliko watu wote duniani. Frederik Mogens alipofika katika helikopta na kukuta Murphy na Yehuda wakihangaika kuutafuta mwili wa Radia, hakushangazwa na walichomwambia. Kwa sababu alijua nini kilitokea. Radia alikutwa akipumua kwa mbali. Hivyo, Debbie na marubani walimchukua na kumpeleka Mexico City haraka ilivyowezekana. Black Hawk waliyokuwa wakiishangaa ilikuwa ya DEA. Lakini si ile waliyokwenda nayo Oaxaca. Ilikuwa nyingine ya DEA, iliyotumwa na Randall Ortega kuwachukua Vijana wa Tume na kuwapeleka Mexico City haraka ilivyowezekana. Black Hawk waliyokwenda nayo Oaxaca ndiyo iliyomchukua Radia na Debbie na kuwapeleka Altamirano (hospitali ya tume) mjini Mexico City. Mogens angekwenda pia na akina Debbie; lakini alibaki kwa ajili ya kumlinda El Tigre, na mizigo yake, na baadhi ya makamanda wake wachache. El Tigre angeweza kutoroka kama angebaki na polisi peke yao, na Mogens hakutaka kufanya makosa.”