Quotessence
Home / Authors / Enock Maregesi Biography

Enock Maregesi Biography

Author

Related Quotes

“Kabla ya uasi, Mungu alimpa Shetani na wasaidizi wake ambao ni mapepo mamlaka makubwa juu ya kila kitu hapa duniani; kuanzia angahewa la dunia hadi ardhi ya dunia nzima nasi wakazi wake tukijumuishwa. Abadani tusisahau kwamba, kwa kiasi kikubwa, kupambana kwetu kama Paulo anavyosema ni dhidi ya hawa mapepo na mfalme wao ambaye ni Shetani. Tunaishi katika eneo ambapo hata wao wanaishi. Hawa mapepo wabaya huwatumia maadui wa msalaba wa Yesu Kristo kutekeleza mipango yao kwa lengo la kuwaangamiza marafiki wote wa msalaba wa Yesu Kristo, wanashawishiwa kwa kiasi kikubwa na hizo mamlaka za kimapepo, na kwa sababu wamedanganywa, hawajui hata kidogo kama Shetani anawatumia! Inawezekana hawajatwaliwa na mapepo lakini wanashawishiwa na mapepo kutenda kinyume na mapenzi ya Mungu kwa wanadamu wote.”

“Jambo ambalo Mungu anataka tulitambue ni kwamba hatuko wenyewe katika bahari hii ya hewa. Hata nyangumi na wazira waovu wanapozunguka huko na huko baharini, ambao pia ni mapepo, wanaochukuliwa kama viumbe wabaya na wachafu na wala mizoga, wanaishi katika bahari hii ya hewa pamoja na sisi. Ni muhimu, kwa ajili ya ustawi wetu wa kiroho, kusikia onyo la Paulo katika Waefeso 6:10-12 kwamba vita yetu si dhidi ya hawa viumbe, na wanapambana usiku na mchana kutetea kile ambacho wanaamini ni cha kwao kwa sababu ya haki ya kuwepo hapa kwanza kabla yetu. Dunia, Biblia inatwambia, ilikuwa makazi yao ya kwanza (Yuda 1:6, KJV). Wanatuchukia kwa sababu taratibu tunakuwa Baba na Mwana, na kwa sababu wanajua hii dunia, urithi wetu, itachukuliwa kutoka mikononi mwao na kukabidhiwa kwa wale ambao ni watoto wa Mungu, wale ambao ni marafiki wa msalaba wa Yesu Kristo.”

“Mbegu tunazopanda leo ni mazao ya msimu ujao. Ukipanda mbegu mbaya utavuna mabaya. Ukipanda mbegu nzuri utavuna mazuri. Ukitenda mabaya leo kesho yako itakuwa mbaya. Ukitenda mazuri leo kesho yako itakuwa nzuri. Okoa kesho leo kwa kupanda mbegu nzuri na kuzimwagilia kwa imani na upendo kwa watu. Mungu ataleta mvua, jua na ustawi wa mazao yako. Panda mbegu ya msamaha kwa maadui zako, uvumilivu kwa wapinzani wako, tabasamu kwa marafiki zako, mfano bora kwa watoto wako, uchapakazi kwa kazi zako, uadilifu kwa waajiri wako na kwa wafanyakazi wako pia kama unao, ndoto kwa malengo yako, na uaminifu kwa marafiki zako wa ukweli. Kila mbegu irutubishwe kwa mapenzi huru yasiyokuwa na masharti yoyote, au mapenzi huru yasiyokuwa na unafiki wa aina yoyote ile. Usifiche vipaji vyako. Ukiwa kimya utasahaulika. Usipopiga hatua utarudi nyuma. Usiwe na hasira, wivu au ubinafsi.”

“Marafiki wanaweza kukupotosha bila wao wenyewe kujua na bila kuwa na nia mbaya ya aina yoyote ile; na wanaweza kuwa washauri wazuri kwa sababu wanakujua vizuri unapokuwa na huzuni, na wanakujua vizuri unapokuwa na furaha pia. Kwa mfano; rafiki yako anaweza kukushauri kusomea uhasibu wakati Mungu amekupangia utawala, au anaweza kujua aongee na wewe wakati gani kulingana na tabia yako ya kubadilikabadilika. Maadui wanasaidia kujua kipaji ulichopewa na Mungu – ukifanya kitu ambacho si cha kawaida katika maisha yako halafu ukawa na maadui ujue hicho ndicho Mungu alichokupangia kufanya, hivyo usikate tamaa – na mashabiki wanasaidia kufanya kipaji chako kiwe na uhai.”

“Maadui ni wazuri kuliko marafiki na mashabiki ni wazuri kuliko maadui. Maadui wanakusaidia kujua wewe ni nani na kwa nini uko hapa. Ukishajua wewe ni nani na kwa nini uko hapa, hakuna mtu atakayekuzuia kufanya chochote unachokiamini zaidi na kukifanya. Chochote unachokiamini zaidi na kukifanya ndicho Mungu alichokupangia kufanya hapa duniani, na kwa sababu hiyo utapata maadui. Ili utoke lazima uwe na mashabiki, marafiki na maadui.”

“Natafuta mwanamke mwenye utu, wema, uaminifu na tabia njema – sifa ambazo ataendelea kuwa nazo hata uzeeni. Sifa hizi zinaweza kubadilika kwa sababu ya maisha au kwa sababu ya mapenzi ya Mungu, lakini mabadiliko haya hayatakuwepo kwa haraka. Sura haidumu. Tabia hudumu.”

“Sina jinsi. Nguzo ya maisha yangu ni historia ya maisha yangu. Historia ya maisha yangu ni urithi wa watu waliojifunza kusema hapana kwa ndiyo nyingi – waliojitolea vitu vingi katika maisha yao kunifikisha hapa nilipo leo – walionifundisha falsafa ya kushindwa si hiari. Siri ya mafanikio yangu ni kujitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu wote; au 'pushing the envelope' kwa lugha ya kigeni.”

“Usimwabudu mungu mwingine isipokuwa Mungu. Usimwabudu mtu, mnyama, sanamu, samaki, au usiziabudu fikira zako kichwani. Usiitumikie kazi, mali, mila, anasa, siasa, wala usiyatumikie mamlaka au usiutumikie umaarufu au ufahari, kuliko Mungu. Ukiithamini kazi, mali, mila, anasa, siasa au ukiyathamini mamlaka, au ukiuthamini umaarufu au ufahari zaidi kuliko Mungu, au ukiyapa majukumu yako muda mwingi zaidi kuliko Mungu umeabudu miungu; wakati ulipaswa kumwabudu Mungu peke yake. Usiwe na vipaumbele vingine vyovyote vile katika maisha yako zaidi ya Mungu, kwani Mungu ni Mungu mwenye wivu.”

“Vita ya Shetani na Mungu inatuathiri zaidi sisi wanadamu – na hapo baadaye itamuathiri Shetani pia. Vita hii haiwezi kuisha hadi siku ya mwisho, Yesu Kristo atakaporudi kuwachukua wateule wake. Pambana kwa njia ya maombi hadi siku ya mwisho kwa sababu adui tunayepambana naye hana muda wa kupumzika. Pambana kujiombea na kuwaombea wengine waliohai, na hata wale ambao bado hawajazaliwa, kabla mafuta ya dunia hii hayajalipuka. Usiishi kama adui wa msalaba wa Yesu Kristo, badala yake, ishi kama rafiki wa msalaba wa Yesu Kristo. Kuishi kama rafiki wa msalaba wa Yesu Kristo ni kupinga majivuno yote ya Shetani kwa upendo uliotukuka wa kujishusha au kujidharirisha, kutokutetereka hata kidogo na tamaa za ulimwengu huu kwa upendo mkubwa wa umaskini, na kutokuyumba wakati wa matatizo kwa sababu wakati wa amani ulijilimbikizia imani.”

“Maarifa unayoyatafuta katika Biblia, Kurani au Yoga ('Oriental Yoga': 'esoteric knowledge': maarifa ya kujua siri ya uumbaji wa Mungu ya 'Kabbalah' ya Kiyahudi au 'Kalachakra' ya Kibudha ya bara la Asia; siri ya sayansi ya kurefusha maisha ya mafundisho ya kiroho ya 'Arcanum' ya Misri – au Kemia ya Mungu au 'Alchemy'; mafundisho ya kiroho ya 'Rosicrucia' ya bara la Ulaya tangu mwishoni mwa karne ya kumi na nne; 'sex magic', 'sex magic' inaweza kukupa utajiri au umaskini hivyo kuwa makini; n.k.) ni hekima na busara. Vingine vyote vitajileta vyenyewe.”

“Maskini na tajiri wana mawazo tofauti. Maskini hudhani utajiri ni chanzo cha matatizo. Tajiri hudhani umaskini ni chanzo cha matatizo. Maskini hudhani ubinafsi ni kitu kibaya. Tajiri hudhani ubinafsi ni kitu kizuri. Maskini ana mawazo ya kupata pesa bila kufanya kazi. Tajiri ana mawazo ya kupata pesa kwa kufanya kazi. Maskini hudhani tajiri ana tabia ya kuringa. Tajiri hupenda kuzungukwa na watu sahihi wenye mawazo sawa na ya kwake. Maskini hutengeneza pesa kwa kufanya kazi asizozipenda. Tajiri hutengeneza pesa kwa kufanya kazi anazozipenda. Maskini hudhani kuwa tajiri lazima usome sana. Tajiri hudhani kuwa tajiri si lazima usome sana. Maskini hutamani mambo mazuri ya wakati uliyopita. Tajiri hutamani mambo mazuri ya wakati unaokuja. Maskini huamini ili uwe tajiri lazima ufanye kitu fulani. Tajiri huamini ili uwe tajiri lazima uwe kitu fulani. Maskini hupenda kuburudishwa kuliko kuelimishwa. Tajiri hupenda kuelimishwa kuliko kuburudishwa. Maskini ana woga. Tajiri hana woga. Maskini hufundisha watoto wake jinsi ya kupambana na maisha. Tajiri hufundisha watoto wake jinsi ya kuwa matajiri. Maskini hana nidhamu ya mapato na matumizi. Tajiri ana nidhamu ya mapato na matumizi. Maskini hufanya kazi kwa bidii kupata pesa. Tajiri hutumia pesa kupata pesa. Maskini ni mdogo kuliko matatizo yake. Tajiri ni mkubwa kuliko matatizo yake. Maskini huamini unahitaji pesa kupata pesa. Tajiri huamini utapata pesa kwa kutumia pesa za wengine. Maskini ana wivu wa chuki. Tajiri ana wivu wa maendeleo. Fikiri kama anavyofikiri tajiri. Ukifikiri tofauti na anavyofikiri tajiri, utakufa maskini.”

“Wape watoto wako urithi wa kutosha ili waweze kufanya kitu, lakini si urithi wa kutosha ili wasiweze kufanya kitu. Wape watoto uhuru wanaostahili kupata, uhuru wa mahesabu, lakini si uhuru wa kila kitu.”

“Heri kuishi kama maskini mwenye pesa nyingi kuliko tajiri mwenye mifuko iliyotoboka, kuliko kusema mbele za watu kwamba pesa haijakupa furaha. Wengi hupata jeuri ya kusema hivyo kutokana na umaskini wa watu wanaowazunguka.”

“Kamishna … karibu," alisema Nafi huku akisimama na kutupa gazeti mezani na kuchukua karatasi ya faksi, iliyotumwa. "Ahsante. Kuna nini …" "Kamishna, imekuja faksi kutoka Oslo kama nilivyokueleza – katika simu. Inakutaka haraka, kesho, lazima kesho, kuwahi kikao Alhamisi mjini Copenhagen," alisema Nafi huku akimpa kamishna karatasi ya faksi. "Mjini Copenhagen!" alisema kamishna kwa kutoamini. "Ndiyo, kamishna … Sidhani kama kuna jambo la hatari lakini." "Nafi, nini kimetokea!" "Kamishna … sijui. Kwa kweli sijui. Ilipofika, hii faksi, kitu cha kwanza niliongea na watu wa WIS kupata uthibitisho wao. Nao hawajui. Huenda ni mauaji ya jana ya Meksiko. Hii ni siri kubwa ya tume kamishna, na ndiyo maana Oslo wakaingilia kati." "Ndiyo. Kila mtu ameyasikia mauaji ya Meksiko. Ni mabaya. Kinachonishangaza ni kwamba, jana niliongea na makamu … kuhusu mabadiliko ya katiba ya WODEA. Hakunambia chochote kuhusu mkutano wa kesho!" "Kamishna, nakusihi kuwa makini. Dalili zinaonyesha hali si nzuri hata kidogo. Hawa ni wadhalimu tu … wa madawa ya kulevya." "Vyema!" alijibu kamishna kwa jeuri na hasira. Halafu akaendelea, "Kuna cha ziada?" "Ijumaa, kama tulivyoongea wiki iliyopita, nasafiri kwenda Afrika Kusini." "Kikao kinafanyika Alhamisi, Nafi, huwezi kusafiri Ijumaa …" "Binti yangu atafukuzwa shule, kam …" "Nafi, ongea na chuo … wambie umepata dharura utaondoka Jumatatu; utawaona Jumanne … Fuata maadili ya kazi tafadhali. Safari yako si muhimu hivyo kulinganisha na tume!" "Sawa! Profesa. Niwie radhi, nimekuelewa, samahani sana. Samahani sana.”

“Israeli ilifikia kikomo cha kipindi chake kikubwa cha mafanikio tangu enzi za Sulemani. Taifa lilikuwa tajiri. Lilikuwa na nguvu. Lilikuwa na silaha nyingi na nzuri zaidi. Lilikuwa taifa lililojidai kwa uwezo wake mkubwa wa nguvu za kijeshi, hekima, ujasiri, utajiri, na faida za kimkakati. Nani angeweza kushindana na Israeli? Lakini Mungu hunguruma onyo kwamba uwezo wote mkubwa wa asili wa taifa, ujuzi waliojipatia, na sifa bora zaidi havikuweza kulisaidia taifa la Israeli. Watu huona nguvu ya taifa katika utajiri wake, idadi yake ya watu, silaha za kijeshi, teknolojia, na maarifa. Lakini Mungu huangalia haki.”

“Mungu alimpa kila mmoja wetu vipawa na vipaji vya pekee kwa ajili ya huduma yake. Kazi yake kwetu hapa duniani ni kutumia vipawa na vipaji vyetu kwa ajili ya huduma ya watu wengine. Kila mmoja wetu ana kitu fulani anachoweza kutoa kwa ajili ya mtu mwingine mwenye shida. Tunaweza kutoa pesa zetu na muda wetu kwa watu maskini. Tunaweza kuwa marafiki kwa watu wapweke au watu wasiojiweza kiafya. Tunaweza kufanya kazi za kujitolea kwa ajili ya mabadiliko ya watu wengine. Tunaweza kuwa wasuluhishi wa migogoro ya amani. Tunaweza kuwa na upendo usiokuwa na masharti yoyote kwa familia zetu. Tunaweza kufanya kazi za kujitolea au kazi za kuajiriwa kwa uadilifu, uaminifu, heshima, na upendo kwa wengine.”

“Musa alipokuwa mlimani kupokea Amri Kumi za Mungu kwa ajili ya Wana wa Israeli alikawia sana kurudi, kiasi cha watu kukata tamaa na kujiona wapweke wakiwa njiani kuelekea katika Nchi ya Ahadi. Kutokana na woga usio na kifani na kukata huko kwa tamaa waliamua kutosubiri tena kusikia neno kutoka kwa Mungu, au kuiona sura halisi ya Mungu kama Musa alivyokuwa amewaahidi, hivyo wakamlazimisha Haruni awatengenezee mungu kutokana na taswira ambayo tayari walishakuwa nayo vichwani mwao kuhusu mungu waliyemtaka; yaani ndama wa dhahabu, au mungu mpya ambaye angewapa chochote walichotaka muda wowote waliotaka.”

“Mwanampotevu dunia ilimfundisha ndiyo maana akarudi kwa baba yake akiwa amenyooka, hakuwa na maadili mema. Yusufu dunia ilimfundisha ndiyo maana akawa waziri mkuu wa Misri, na ndiyo maana akaokoa familia yake kutokana na njaa, alikuwa na maadili mema. Heri kudharaulika kwa kutenda mema kuliko kudharaulika kwa kutenda maovu. Ukidharaulika kwa kutenda maovu hutaishi sawasawa na mapenzi ya Mungu. Ukidharaulika kwa kutenda mema Mungu atakuinua.”