Quotessence
Home / Authors / Enock Maregesi

Enock Maregesi Quotes

Author

Filter quotes by topic

Famous Enock Maregesi Quotes

“Marafiki wanaweza kukupotosha bila wao wenyewe kujua na bila kuwa na nia mbaya ya aina yoyote ile; na wanaweza kuwa washauri wazuri kwa sababu wanakujua vizuri unapokuwa na huzuni, na wanakujua vizuri unapokuwa na furaha pia. Kwa mfano; rafiki yako anaweza kukushauri kusomea uhasibu wakati Mungu amekupangia utawala, au anaweza kujua aongee na wewe wakati gani kulingana na tabia yako ya kubadilikabadilika. Maadui wanasaidia kujua kipaji ulichopewa na Mungu – ukifanya kitu ambacho si cha kawaida katika maisha yako halafu ukawa na maadui ujue hicho ndicho Mungu alichokupangia kufanya, hivyo usikate tamaa – na mashabiki wanasaidia kufanya kipaji chako kiwe na uhai.”

“Natafuta mwanamke mwenye utu, wema, uaminifu na tabia njema – sifa ambazo ataendelea kuwa nazo hata uzeeni. Sifa hizi zinaweza kubadilika kwa sababu ya maisha au kwa sababu ya mapenzi ya Mungu, lakini mabadiliko haya hayatakuwepo kwa haraka. Sura haidumu. Tabia hudumu.”

“Sina jinsi. Nguzo ya maisha yangu ni historia ya maisha yangu. Historia ya maisha yangu ni urithi wa watu waliojifunza kusema hapana kwa ndiyo nyingi – waliojitolea vitu vingi katika maisha yao kunifikisha hapa nilipo leo – walionifundisha falsafa ya kushindwa si hiari. Siri ya mafanikio yangu ni kujitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu wote; au 'pushing the envelope' kwa lugha ya kigeni.”

“Maarifa unayoyatafuta katika Biblia, Kurani au Yoga ('Oriental Yoga': 'esoteric knowledge': maarifa ya kujua siri ya uumbaji wa Mungu ya 'Kabbalah' ya Kiyahudi au 'Kalachakra' ya Kibudha ya bara la Asia; siri ya sayansi ya kurefusha maisha ya mafundisho ya kiroho ya 'Arcanum' ya Misri – au Kemia ya Mungu au 'Alchemy'; mafundisho ya kiroho ya 'Rosicrucia' ya bara la Ulaya tangu mwishoni mwa karne ya kumi na nne; 'sex magic', 'sex magic' inaweza kukupa utajiri au umaskini hivyo kuwa makini; n.k.) ni hekima na busara. Vingine vyote vitajileta vyenyewe.”

“Maskini na tajiri wana mawazo tofauti. Maskini hudhani utajiri ni chanzo cha matatizo. Tajiri hudhani umaskini ni chanzo cha matatizo. Maskini hudhani ubinafsi ni kitu kibaya. Tajiri hudhani ubinafsi ni kitu kizuri. Maskini ana mawazo ya kupata pesa bila kufanya kazi. Tajiri ana mawazo ya kupata pesa kwa kufanya kazi. Maskini hudhani tajiri ana tabia ya kuringa. Tajiri hupenda kuzungukwa na watu sahihi wenye mawazo sawa na ya kwake. Maskini hutengeneza pesa kwa kufanya kazi asizozipenda. Tajiri hutengeneza pesa kwa kufanya kazi anazozipenda. Maskini hudhani kuwa tajiri lazima usome sana. Tajiri hudhani kuwa tajiri si lazima usome sana. Maskini hutamani mambo mazuri ya wakati uliyopita. Tajiri hutamani mambo mazuri ya wakati unaokuja. Maskini huamini ili uwe tajiri lazima ufanye kitu fulani. Tajiri huamini ili uwe tajiri lazima uwe kitu fulani. Maskini hupenda kuburudishwa kuliko kuelimishwa. Tajiri hupenda kuelimishwa kuliko kuburudishwa. Maskini ana woga. Tajiri hana woga. Maskini hufundisha watoto wake jinsi ya kupambana na maisha. Tajiri hufundisha watoto wake jinsi ya kuwa matajiri. Maskini hana nidhamu ya mapato na matumizi. Tajiri ana nidhamu ya mapato na matumizi. Maskini hufanya kazi kwa bidii kupata pesa. Tajiri hutumia pesa kupata pesa. Maskini ni mdogo kuliko matatizo yake. Tajiri ni mkubwa kuliko matatizo yake. Maskini huamini unahitaji pesa kupata pesa. Tajiri huamini utapata pesa kwa kutumia pesa za wengine. Maskini ana wivu wa chuki. Tajiri ana wivu wa maendeleo. Fikiri kama anavyofikiri tajiri. Ukifikiri tofauti na anavyofikiri tajiri, utakufa maskini.”

“Wape watoto wako urithi wa kutosha ili waweze kufanya kitu, lakini si urithi wa kutosha ili wasiweze kufanya kitu. Wape watoto uhuru wanaostahili kupata, uhuru wa mahesabu, lakini si uhuru wa kila kitu.”

“Hakuna mtu mwenye akili timamu anayetaka mabaya katika maisha yake. Mwanamume atake mwanamke mwenye matendo mema. Mwanamke atake mwanamume mwenye matendo mema. Misingi ya hasanati ni misingi ya utu. Tukiishi katika misingi ya utu, misingi ya matendo mema, tutaishi sawasawa na mapenzi ya Mungu. Kila mtu anapaswa kuishi na mke au mume aliye mwema.”

“Wazazi wetu ni watu wa kuheshimu kuliko kitu kingine chochote kile kwa sababu wana uwezo wa kuona tusipoweza kuona. Yaani, wanajua kilichokuwepo kabla ya sisi kuzaliwa na wanajua kilichokuwepo baada ya sisi kuzaliwa. Maisha tuliyopitia, wazazi wetu walishapitia. Tulipokuwa, wazazi wetu walishakuwepo; na tulichofanya, wazazi wetu walishafanya. Hivyo, hatuna budi kuwaheshimu wazazi wetu. Lakini, wazazi wetu wanapaswa kujiheshimu kutufundisha adabu na maadili mema.”

“Nilijifunza toka awali umuhimu wa kushindwa katika maisha ijapokuwa nilijitahidi sana, na nilipoendelea kushindwa niliweka nadhiri ya kufanya kitu kimoja kilicholeta maana zaidi katika maisha yangu nacho ni uandishi wa vitabu. Uandishi wa vitabu ndicho kitu pekee nilichokiweza zaidi kuliko vingine vyote na kuanzia hapo Mungu aliniweka huru. Nilijua mimi ni nani. Nilijua kwa nini nilizaliwa. Nilijifunza falsafa ya kuacha dunia katika hali nzuri kuliko nilivyoikuta – kwa sababu hata mimi nilikuwepo – na falsafa ya kushindwa si hiari. Maarifa hayo yakafanya niwe na heshima na upendo kwa watu wote.”

“Lakini damu na maji vina maana kubwa katika maisha yetu. Biblia inaeleza kuwa wakati Yesu Kristo akiwa msalabani alichomwa ubavu wake kwa mkuki, ikatoka damu na maji, ndipo zilipozaliwa sakramenti za kanisa. Aidha, tukio la askari wa Kirumi kumchoma Yesu na damu na maji kutoka lina maana nyingine kubwa katika maisha yetu. Hapo ndipo Ukristo ulipozaliwa; na ni kwa sababu hiyo mwanamke anapojifungua hutoa damu na maji kutokana na kupasuka kwa utando wa mfuko wa uzazi. Kutokana na hayo, Wakristo wanapoabudu msalaba wanaeleza umuhimu wa matukio na mafundisho waliyopata kupitia mateso aliyopata kiongozi wao na kuwa, msalaba ni chombo cha ukombozi.”

“Mungu hutumia watu 'wajinga' na 'wapumbavu' kufanya mambo makubwa katika maisha yao na ya watu wengine. Katika Biblia, Musa aliitwa mjinga alipokiuka amri ya Farao ya kuendelea kuwafanya watumwa wana wa Israeli nchini Misri; Nuhu aliitwa mpumbavu alipohubiri kwa miaka mia kuhusu gharika, katika kipindi ambacho watu hawakujua mvua ni nini; Daudi aliitwa mjinga alipojitolea kupambana na Goliati bonge la mtu, shujaa wa Gathi; Yusufu aliitwa mjinga alipokataa kulala na mke wa bosi wake, baada ya kuwa ameuzwa na nduguze kama mtumwa nchini Misri; Abrahamu aliitwa mjinga alipoamua kuhama nchi aliyoipenda na kwenda katika nchi ya ahadi, eti kwa sababu Mungu alimwambia kufanya hivyo; Yesu aliitwa mjinga mpaka akasulubiwa aliposema yeye ni Mfalme na Mwana wa Mungu. LAKINI, Musa alitenganisha Bahari ya Shamu na kuwapeleka Waisraeli katika nchi ya ahadi, ambako aliwakomboa kutoka utumwani. Nuhu aliokoa dunia. Daudi alimshinda Goliati. Yusufu aliokoa familia yake kutokana na njaa. Abrahamu alikuwa baba wa imani. Yesu aliyashinda mauti. Wakati mwingine tunatakiwa kufanya mambo makubwa kulingana na jinsi Roho Mtakatifu anavyotutuma, bila kujali watu au dunia itasemaje.”

“Nyota ni kipaji, kipawa, takdiri, karama, au uweza; ni kiashiria cha rohoni kinachoonyesha mtu atakuwa nani baadaye, mafanikio ya mtu, au takdiri ya maisha ya mwanadamu. Unabii na nyota ya ufalme ni kibali cha Mungu katika maisha ya mtu. Kupata kibali hicho, tembea na watu sahihi katika maisha yako (tembea na watu ambao Mungu amekuchagulia kushika funguo za takdiri ya maisha yako). Tamka na kukiri kibali cha Mungu katika maisha yako yote. Panda mbegu za kibali cha Mungu katika udongo wa maisha yako. Jifunze kutenda mema bila malipo, kwani wema ni mbegu ya kibali cha Mungu. Jali mambo ya ufalme wa Mungu.”

“Kila binadamu hapa duniani ni wa thamani kubwa. Chochote utakachofanya, kizuri au kibaya, kidogo au kikubwa, kitabadilisha maisha ya watu. Ukiwa na msingi mzuri kwa mwanao ataishi vizuri atakapokuwa mkubwa, atakuwa na uwezo mkubwa wa kuacha dunia katika hali nzuri kuliko alivyoikuta. Ukiwa na msingi mbaya kwa mwanao ataishi vibaya atakapokuwa mkubwa, atakuwa na uwezo mdogo wa kuacha dunia katika hali nzuri kuliko alivyoikuta. Kuwa mkarimu kwa mazingira, kuwa mkarimu kwa wanyama, kuwa mkarimu kwa binadamu wenzako, kwa faida ya vizazi vijavyo.”

“Siri ya utajiri ni mawazo ya mtu. Maisha unayoishi uliyataka mwenyewe. Amka uishi. Hii ndiyo siri kubwa ya utajiri kuliko zote ulimwenguni. Ukifikiria chanya maisha yako yatakuwa chanya, ukifikiria hasi maisha yako yatakuwa hasi. Unachofikiria ndicho unachokuwa. Siri ya mafanikio yako ni jumla ya mambo unayoyawaza.”

“Kutakuwepo na nguvu za chanya na hasi katika maisha yako kadiri utakavyoishi hapa duniani. Ukiruhusu moyo wako kuwa chanya utakuwa chanya. Ukiruhusu moyo wako kuwa hasi utakuwa hasi. Shetani hawezi kuona ndani ya moyo wako mpaka wewe mwenyewe umwonyeshe. Ukionyesha chanya Mungu atakupa chanya. Ukionyesha hasi Shetani atakupa hasi.”

“Nukuu ya mwandishi wa vitabu wa Brazili, Paulo Coelho, "Tunapopenda tunajitahidi siku zote kuwa wazuri zaidi kuliko jinsi sisi wenyewe tulivyo. Tunapojitahidi kuwa wazuri zaidi kuliko jinsi sisi wenyewe tulivyo, kila kitu katika maisha yetu kinakuwa kizuri hali kadhalika.", inadhihirisha kikamilifu tabia ambayo bibi yangu (Martha Maregesi) alijitahidi kuwa nayo katika kipindi cha maisha yake yote. Alikuwa mtu mwenye furaha sana. Alikuwa na tabasamu lenye kuambukiza ambalo marafiki na familia yake hawakuweza kujizuia kutabasamu pia alipofurahi nao. Pamoja na kwamba alikumbana na matatizo mengi na bahati mbaya nyingi katika maisha yake, alijulikana kama mtu mwenye upendo na uvumilivu mkubwa.”

“Maombi ya sifa huunganisha watu wa Mungu na hutayarisha njia kwa ajili ya uwezo wa Mungu katika maisha yetu. Thamani ya maombi ya sifa wakati wa matatizo ni kuimarisha imani yetu, na kuwa karibu na Mungu wetu. Mungu anataka tumpe sifa na kumshukuru kwa kila jambo, kama Mtume Paulo anavyosema katika waraka wa kwanza wa Wathesalonike 5:16-18. Kumshukuru Mungu wakati wa matatizo ni amri, si ombi.”

“Nini kingetokea kama Adamu na Hawa wasingekula tunda la Mti wa Maarifa ya Mema na Mabaya mpaka siku ya Sabato? Mungu angewaruhusu kula na lengo la uumbaji wa Mungu lingekamilika. Wanadamu wakifuata Amri Kumi za Mungu katika maisha yao watakuwa na uwezo maalumu ambao baadaye utawawezesha, kupitia Roho Mtakatifu, kuwa na maarifa ya siri ya uumbaji wa Mungu.”

“Usiingilie mambo ya mtu mwingine bila kibali kutoka kwa Mungu. Kuingilia mambo ya mtu mwingine bila kibali kutoka kwa Mungu ni dhambi. Dhambi hiyo itakuathiri. Hivyo, jali mambo yako – ya mwingine Mungu anayafanyia kazi – hadi utakapoitwa na Mungu kuingilia kati. Kuingilia kati mambo ya mtu mwingine kunaweza kuathiri mpango wa Mungu katika maisha yake. Hivyo, acha.”

“Wewe kuingilia mambo ya John ni sawa na kusema, ‘Mungu umeshindwa hebu ngoja na mimi nijaribu; ngoja niingilie kati kukusaidia juu ya maisha ya John Doe.’ Hiyo ni dhambi. Tena ni dhambi kubwa. Unajifananisha na Mungu; kwamba Mungu wa John Doe ameshindwa kwa hiyo mungu wewe ndiye utakayemtatulia matatizo yake. Amri kuu ya kwanza ya Mungu inasema, ‘Usiwe na miungu mingine ila mimi.’ Kuingilia mambo ya John tayari umevunja amri ya kwanza ya Mungu kwa kujifanya Mungu. Mungu ana mpango na maisha ya John, na anatumia matatizo yake kumfikisha kwenye takdiri aliyompangia. Hivyo, wewe si Mungu, acha Mungu afanye kazi yake. Mungu akikuruhusu kuingilia kati, yaani John akiamua kwa hiari yake mwenyewe kukuomba msaada wa mawazo au ushauri, maana yake ni kwamba Mungu amekuchagua wewe kuwa sehemu ya mafanikio ya John Doe.”

“Mungu alimuumba mwanadamu ili aitawale dunia. Shetani tayari alikuwepo wakati Adamu anaumbwa. Adamu na Hawa walipokula tunda la mti wa katikati, walikufa kiroho – Yaani, walipoteza sura na asili ya Mungu – Shetani akawashinda kuanzia kipindi hicho na kuendelea. Tulizaliwa katika dhambi. Kila mtu anayezaliwa anazaliwa katika dhambi. Njia pekee ya kuikomboa sura na asili ya Mungu ni kumpokea Yesu (Kristo) kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako.”

“Kuna vita za aina mbili zinazopiganwa hapa duniani: vita ya maisha na vita ya dhambi. Unaweza kushinda vita ya maisha (maisha ya raha) lakini ukashindwa vita ya dhambi (maisha ya laana). Kushinda vita ya dhambi ni lazima umkaribishe Mwana wa Mungu Mfalme wa Amani, Yesu Kristo wa Nazareti Aliye Hai, kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako.”

“Vita ya dhambi hupiganwa katika uwanja wa akili na katika uwanja wa mwili kati ya Shetani na Mungu. Hutumia silaha kuu ya uongo na silaha kuu ya ukweli. Mungu anataka tuujue ukweli. Shetani anataka tuujue uongo. Kushinda vita ya dhambi huna budi kutumia neno la Mungu, kama Yesu alivyolitumia kumshinda Shetani wakati akijaribiwa katika Mlima wa Majaribu wa Jangwa la Yuda.”

“Radia hakuwa na makosa. Wengi huishi maisha yao bure. Yeye aliishi ya kwake kwa ajili ya watu. Hakuishi tu kama raia wa Tunisia. Aliishi kama raia wa uanadamu, maadili mema na uchapakazi. Watu walimsifu kwa kuwa na kaulimbiu ya 'Acha dunia katika hali nzuri kuliko ulivyoikuta'.”

“Katika maisha watu wengi hawataki kukuona ukiendelea kwa sababu ukiendelea unakuwa kioo kwao. Ghafla wataanza kukutazama. Wanajua wana akili kama wewe, wamesoma kama wewe, au wana akili kuliko wewe, au wamesoma kuliko wewe, na labda wanazijua sifa zako za udhaifu na sifa zako za ushupavu toka utotoni kwako. Lakini ghafla unakuwa kioo, na wanapojitazama katika hicho kioo, wanajiona taswira zao isipokuwa sasa hawapo mahali ambapo wewe upo. Katika maisha watu watakushauri, watakufitini, watakurubuni na watakukatisha tamaa. Sema hapana kwa ndiyo nyingi kwa sababu hawaoni unachokiona, hawajui unachokifanya na hawajui unapoelekea. Unachokiona ni takdiri ya maisha yako, unachokifanya ni kupanda mbegu na kuzimwagilia kwa imani, na unapoelekea ni kileleni. Hivyo, songa mbele, kuwa wewe daima, wape muda, wape nafasi.”

“Kinachotokea katika dunia hii si kitu kizuri cha kuzoea au hata kufikiria. Hivyo tuna haki ya kuwa na mawazo, hasira na wanyonge kuhusiana na suala zima la maisha yetu hapa duniani. Hata hivyo hali hii itabaki kuwa hivyo kwa sababu Mungu ametaka iwe hivyo kwa sasa. Kwa maana hiyo, hekima ni kukubaliana na mapenzi ya Mungu. Lazima tukubaliane na kisichoweza kufikirika kuweza kubadilika.”

“Maamuzi ya Adamu na Hawa ya kutokumtii Mungu juu ya Mti wa Maarifa ya Mema na Mabaya, ndiyo yaliyosababisha Yesu Kristo ajitolee maisha yake ili wengine waweze kuishi. Hakuna Mungu bila Yesu. Mtafute Yesu, kukomboa sura na asili ya Mungu.”

“Kila mmoja wetu ana kitu cha kutoa. Wengine wana pesa, wengine wana vipaji, wengine wana muda. Vipaji vyote tulivyopewa na Mungu, vikubwa au vidogo, hatuna budi kuvitumia kiukarimu kwa watu wanaovihitaji. Tunapofanya hivyo tunaleta mabadiliko katika dunia kwa ajili ya watu fulani, na tunapata maana halisi ya maisha na toshelezo la moyo katika maisha yetu.”

“Wakati mwingine inaweza kuonekana kuwa kadiri unavyozidi kujitolea kwa ajili ya watu wengine ndivyo unavyozidi kuwa maskini, lakini hii si kweli. Huduma kwa ajili ya watu wengine huleta maana fulani na ukamilifu katika maisha yetu kwa namna ambayo utajiri, madaraka na mali haviwezi kushindana nao. Mungu hababaishwi na kiasi gani unatoa. Anababaishwa na imani uliyonayo wakati unatoa. Ukitoa kidogo inatosha. Ukitoa kingi inatosha pia.”

“Siri ya mafanikio yako ni chumba chako. Dali linasema anga ndicho kipimo cha kufikiria; Dirisha linasema utazame nje uone fursa zilizopo ulimwenguni; Feni linasema uwe mtulivu usikurupuke kufanya lolote; Kalenda inasema uwe mtu anayekwenda na wakati; Kioo kinasema ujitazame na ujiamini kabla ya kutenda lolote; Kitabu cha dini kinasema unapaswa kumwamini Mungu ili uishi; Kitanda kinasema ujifunze kuwa na likizo; Mlango unasema usipitwe na fursa ya aina yoyote ile hapa duniani; Saa inasema kila sekunde ina thamani sana katika maisha yako hivyo tumia muda wako vizuri. Amka uishi.”

“Badilisha tabia. Badilisha mazingira ya maisha yako. Haijalishi una umri kiasi gani au wewe ni mwanamke au mwanamume, bado hujachelewa kubadili maisha yako kutoka duni kuwa bora – kuwa na amani, furaha na kuridhika. Kama desturi yako ni kuamka saa 12:00 asubuhi kila siku ili ufike kazini saa 2:00 asubuhi ambao ni muda wa serikali wa kuanza kazi, amka saa 11:30 asubuhi ili ufike kazini saa 1:30 asubuhi – nusu saa kabla ya kuanza kazi. Kama unafanya kazi ya taaluma uliyosomea lakini maisha hayaendi, fikiria kubadili mwelekeo wa maisha ikiwemo taaluma kufikia malengo uliyojiwekea.”