Quotessence
Home / Authors / Enock Maregesi

Enock Maregesi Quotes

Author

Filter quotes by topic

Famous Enock Maregesi Quotes

“Usimwabudu mungu mwingine isipokuwa Mungu. Usimwabudu mtu, mnyama, sanamu, samaki, au usiziabudu fikira zako kichwani. Usiitumikie kazi, mali, mila, anasa, siasa, wala usiyatumikie mamlaka au usiutumikie umaarufu au ufahari, kuliko Mungu. Ukiithamini kazi, mali, mila, anasa, siasa au ukiyathamini mamlaka, au ukiuthamini umaarufu au ufahari zaidi kuliko Mungu, au ukiyapa majukumu yako muda mwingi zaidi kuliko Mungu umeabudu miungu; wakati ulipaswa kumwabudu Mungu peke yake. Usiwe na vipaumbele vingine vyovyote vile katika maisha yako zaidi ya Mungu, kwani Mungu ni Mungu mwenye wivu.”

“Hakuna mtu mwenye akili timamu anayetaka mabaya katika maisha yake. Mwanamume atake mwanamke mwenye matendo mema. Mwanamke atake mwanamume mwenye matendo mema. Misingi ya hasanati ni misingi ya utu. Tukiishi katika misingi ya utu, misingi ya matendo mema, tutaishi sawasawa na mapenzi ya Mungu. Kila mtu anapaswa kuishi na mke au mume aliye mwema.”

“Hasira ni Shetani. Hekima ni Mungu. Kila kitu kimo ndani yetu. Hasira imo ndani yetu. Hekima imo ndani yetu. Atomu ni matofali ya ujenzi wa kila kitu ulimwenguni likiwemo jua na miili ya wanadamu. Ndani ya atomu kuna nguvu ya chanya na kuna nguvu ya hasi. Kama miili yetu imetengenezwa na atomu na katika kila atomu kuna nguvu ya chanya na kuna nguvu ya hasi, hivyo basi, tuna uwezo mkubwa wa kufanya mambo mazuri na tuna uwezo mkubwa wa kufanya mambo mabaya. Mtu akikutukana mwambie asante. Akikupiga mwambie asante. Akiendelea kukupiga, pigana. Geuza hasira yako kuwa hekima kwa faida yako na kwa faida ya wengine.”

“Palestina ni nchi ya Waisraeli waliyopewa na Mungu wa Yakobo. Hata hivyo, hawakutimiza masharti. Mungu aliwaagiza kuua kila mtu katika nchi ya Kaanani na miji yake yote. Waisraeli, wakiongozwa na Yoshua, waliua watu wengi katika nchi ya Kaanani. Hawakuua kila mtu katika miji ya Ashdodi, Gathi na Ukanda wa Gaza kama walivyoagizwa. Mungu alimwambia Ibrahimu kuwa angempa yeye na uzao wake nchi ya Kaanani kuwa milki yao ya milele, na kuwa Yeye ndiye angekuwa Mungu wao daima. Vita ya Israeli na Palestina itamalizwa na Mungu. Itamalizwa na hekima.”

“Nyota ni kipaji, kipawa, takdiri, karama, au uweza; ni kiashiria cha rohoni kinachoonyesha mtu atakuwa nani baadaye, mafanikio ya mtu, au takdiri ya maisha ya mwanadamu. Unabii na nyota ya ufalme ni kibali cha Mungu katika maisha ya mtu. Kupata kibali hicho, tembea na watu sahihi katika maisha yako (tembea na watu ambao Mungu amekuchagulia kushika funguo za takdiri ya maisha yako). Tamka na kukiri kibali cha Mungu katika maisha yako yote. Panda mbegu za kibali cha Mungu katika udongo wa maisha yako. Jifunze kutenda mema bila malipo, kwani wema ni mbegu ya kibali cha Mungu. Jali mambo ya ufalme wa Mungu.”

“Pesa ina thamani pale unapokuwa nayo, si pale unapokuwa huna, hivyo iweke mahali unapoweza kuiona: katika nyumba, katika shamba au katika elimu. Badala ya kumpa mtu pesa ili ajenge nyumba, mpe nyumba. Badala ya kumpa mtu pesa ili afanye biashara, mpe biashara. Halafu, mpe elimu afanye maamuzi ya biashara yake. Pesa ina laana na Mungu pekee ndiye anayeweza kuiondoa laana hiyo. Ni rahisi kwa tajiri kupata baraka ya pesa kwa sababu ana pesa na ana uwezo mkubwa wa kusaidia maskini. Ni vigumu kwa maskini kupata baraka ya pesa kwa sababu hana au ana uwezo mdogo wa kusaidia maskini. Mungu anaweza kuondoa laana ya pesa kupitia hisani kwa maskini, kitu ambacho aghalabu hufanywa na matajiri wenye uwezo mkubwa. Heri kutoa kitu au huduma au elimu kwa maskini kuliko pesa.”

“Kuna vitu vitatu ndani ya mtu: kuna hiari, kuna ufahamu, na kuna mwili. Hiari inatawaliwa na Mungu; ufahamu unatawaliwa na malaika mwema; mwili unatawaliwa na nyota lakini chini ya usimamizi wa malaika wema: malaika wema walisimamisha jua na mwezi kwa ajili ya Yoshua na wana wa Israeli juu ya Gibeoni na katika bonde la Aiyaloni, walirudisha jua nyuma kwa ajili ya Hezekia mfalme wa Yuda na kwa ajili ya nabii Isaya, na waliifanya dunia ‘kuvaa koti’ ghafla wakati wa kusulubiwa kwa Mwanakondoo wa Mungu Anayeondoa Dhambi. Moyoni ni mahali patakatifu. Hata malaika wema hawawezi kuona ndani ya moyo wa mtu, ni Mungu pekee mwenye uwezo wa kufanya hivyo, na alichokihifadhi Mungu ndani ya moyo huo ni hiari ya mtu ya kuchagua mema au mabaya.”

“Mapenzi, kama ilivyo kwa vitu vyote hapa ulimwenguni, hayawezi kuwepo bila kujumuishwa na fizikia na kemia yake! Bila kemia hakuna mapenzi ya kudumu. Tamaa ya ngono kimsingi huanza pindi unapokutana na mtu. Tamaa hiyo huweza kukua na kuwa kitu kingine kadiri muda unavyokwenda lakini chanzo kinakuwepo toka siku ya kwanza mlipokutana. Kemikali inayosababisha tamaa ya ngono na hata kuikuza tamaa hiyo ni 'phenyl ethylamine' ('fino itholamine') au PEA ambayo ni kemikali ya mapenzi ndani ya ubongo. Husisimua watu na huongeza nguvu za kimwili (fizikia) na kihisia (kemia). Tamaa husababisha mtu azalishe PEA nyingi zaidi, kitu kinachosababisha kujisikia kizunguzungu (cha hisia za kimapenzi) na dalili zingine kama magoti kutetemeka, jasho kutoka viganjani na kutokutulia. Kemikali hii inapozalishwa kwa kiwango kikubwa, hutuma alamu ('signals') kutoka kwenye ubongo mpaka kwenye viungo vingine vya mwili na kutumika kama 'dopamine' au 'amphetamine' ambazo ni kemikali za ulevi ndani ya ubongo. Iwapo unajiuliza kwa nini wewe au mtu mwingine unavutiwa na mtu ambaye hamwendani kimapenzi, inaweza kuwa ni kwa sababu una kiwango kikubwa cha kemikali hizo kuliko mwenzako, kitu ambacho huzidi uwezo wa kutumia kichwa na kutoa maamuzi bora kulingana na akili ya kuzaliwa. Kwa jumla, mapenzi yote ya kweli uhitaji angalau kiwango kidogo cha PEA kwa wale wanaopendana. Cha msingi kukumbuka ni kwamba kemikali hizi huja kwa vituo, nikiwa simaanishi kwamba tamaa ya ngono hupotea pale mtu anapoelekea kwenye uhusiano wa kudumu. Lakini mambo hubadilika. Hatuwezi kuvumilia zile hisia kali kadiri tunavyozidi kusafiri kuelekea kwenye uhusiano wa kudumu na kwenye maisha ya pamoja yenye furaha. Katika uhusiano wenye afya hata hivyo matatizo hutokea hapa na pale. Chanzo cha Murphy na Debbie kupendana kilikuwa kemia zaidi kuliko fizikia. Kama hakuna kemia hakuna mapenzi.”

“Kila mtu ana tabia, matendo, mawazo na akili yake tofauti na mtu mwingine hapa duniani. Usimdharau mtu ukidhani ana akili kama za kwako au anafikiri kama unavyofikiri wewe kwani kila mtu aliumbwa kivyake na Mwenyezi Mungu. Unaweza kudhani unamjua mtu kumbe humjui. Heshimu kila mtu kama unavyojiheshimu kwa sababu, kila mtu ni wa pekee. Kama tunavyotofautiana katika vidole na macho ndivyo tunavyotofautiana katika tabia, matendo, mawazo, imani, maadili na akili. Usimdharau mtu usiyemjua au unayedhani unamjua.”

“Ukiua mtu bila kumwambia kwa nini unamuua anaweza kujua umemuua kwa kumwonea. Akijua umemuua kwa kumwonea roho yake inaweza kukusumbua wewe na familia yako maisha yenu yote. Makachero wa EAC wana leseni ya kuua. Lakini si kuua ovyo kama James Bond. Kila wanayemuua lazima waandike ripoti kwa nini wamemuua. Kachero wa EAC akiua mtu, kwa makosa, kwa bahati mbaya, atalindwa na Mwenyezi Mungu. Atalindwa na Tambiko la Tume ya Dunia.”

“Msamaha ni uamuzi wa makusudi wa kuachilia hisia za chuki au kisasi juu ya mtu au kikundi cha watu ambaye amekuumiza au ambacho kimekuumiza, bila kujali kama anastahili au kinastahili msamaha wako. Wataalamu wanaosoma au kufundisha msamaha huweka bayana ya kuwa, unaposamehe, hutakiwi kusitiri au kukana uzito wa kosa ulilofanyiwa. Msamaha haumaanishi kusahau wala haumaanishi kupuuza, au kujisingizia, makosa ambayo mtu amekufanyia au kikundi cha watu kimekufanyia. Ijapokuwa msamaha unaweza kusaidia kujenga uhusiano ulioharibika, haukulazimishi kupatana na mtu aliyekukosea au kumfanya asiwajibike kisheria kwa makosa aliyokufanyia. Badala yake, msamaha humletea yule anayesamehe amani ya moyo; na humpa uhuru kutokana na hasira aliyokuwa nayo, juu ya yule aliyemkosea.”

“Tunazaliwa, kuteseka na kufa kwa sababu ya dhambi ya asili ya wazazi wetu wa kwanza (Adamu na Hawa). Kama Hawa asingekubali kudanganywa na Shetani, tungezaliwa bila uchungu, tungeishi bila kuteseka na tusingekufa milele. Lakini haya ndiyo mawazo yangu: Mungu Ahusiki na dhambi, Ahusiki na mwili, Anahusika na roho. Hivyo, mtu anapofariki mwili unabaki duniani lakini roho inarudi kwa Mungu; kwani Yeye ndiye aliyeitengeneza na kuiweka katika moyo wa mtu. Mimi na wewe ni viumbe vyenye thamani kubwa sana mbele za Mwenyezi Mungu; mapenzi Yake kwetu hayana masharti yoyote. Hainiingii akilini (hata kidogo) kumtesa mtu unayempenda kiasi hicho milele, wakati uwezo wa kumwokoa unao.”

“Kuna ndoto za mchana na kuna ndoto za usiku. Ndoto za mchana ni maono ya kile ambacho roho inatamani kuwa. Ndoto za usiku ni maono yanayotokea wakati akili imetulia baada ya mwili wote kupumzika. Ukiota kuhusu moto, hiyo ni ishara ya hasira; ukiota kuhusu maji, hiyo ni ishara ya siri; ukiota kuhusu ardhi, hiyo ni ishara ya huzuni; ukiota kuhusu Yesu, hiyo ni ishara ya mafanikio. Kitu cha kwanza kufanya unapoota ndoto za kishetani, utakapoamka, mwombe Mungu akunusuru kutoka katika matatizo yoyote yanayokunyemelea; au yanayomnyemelea mtu mwingine yoyote yule, hata usiyemjua. Ubongo ni kitu cha ajabu kuliko vyote ulimwenguni na umetengenezwa na Mungu. Ndoto zinapatikana ndani ya ubongo. Ubongo unapatikana ndani ya ufahamu. Ufahamu mtawala wake ni malaika mwema. Malaika mwema anajua siri ya ndoto. Kila mtu anaota na kila ndoto ina maana yake. Rekodi ndoto zako kila siku kwa angalau mwezi mzima kupata maana halisi ya ndoto hizo, na kujua kwa nini ulizaliwa.”

“Ikiwa huna pesa na una mke na watoto kwa mfano, mke wako (wanawake walio wengi) hatakuona wa maana kwa sababu ya ustawi wa maisha ya familia yake. Ikiwa una mwanamke asiyekuwa na busara au hekima ya kutosha, au mwanamke ambaye akili zake zimefyatuka kidogo, atakusaliti kutafuta bwana au mtu mwenye maana. Kama huna pesa huna maana kwa mwanamke.”

“Kamera ina athari kubwa sana katika maisha yetu. Inaweza kuharibu taswira ya mtu mbele ya jamii, na inaweza kuharibu maisha ya mtu hali kadhalika. Wasanii wakubwa duniani hawatoki ndani bila ya kuwa nadhifu au bila ya kujipodoa. Kwa nini? Kwa sababu ya wasanii wao wa vipodozi. Wasanii wao wa vipodozi hawataki waajiri wao wawe na taswira mbaya mbele ya wateja wao ambayo ni jamii. Kuwa na taswira mbaya mbele ya jamii kunaweza kusababisha wao (wasanii wa vipodozi) pamoja na waajiri wao, wasiishi vizuri hapa duniani kama wanavyotaka. Kioo ni kitu au mtu. Kama huna uwezo wa kumiliki vipodozi, miliki kioo. Kama huna uwezo wa kumiliki kioo, miliki rafiki. Kioo (hasa kitu) hakina unafiki. Usitoke ndani bila kuridhika na taswira yako.”

“Wataalamu wanaosoma au kufundisha msamaha huweka wazi kwamba unapomsamehe mtu, huwezi kupotezea au kukana uzito wa kosa alilokufanyia. Kusamehe ni hali fulani inayotoka ndani ya moyo wa mtu, ikiwa na hali ya uhuru wa hiari wa mtu mwenyewe kuamua kuachilia kile kinachomuumiza, pasipo kuwepo masharti ya aina yoyote ile kwa mtu aliyemuumiza.”

“Mwili wako una uwezo wa kujua kabla yako kitakachotokea baadaye. Kama una njaa kwa mfano, mwili wako utakwambia. Kama una kiu, mwili wako utakwambia. Kama unaumwa, mwili wako utakwambia. Kama kuna kitu kibaya kinatarajia kutokea katika maisha yako au katika maisha ya mtu mwingine, mwili wako utakwambia. Kuwa makini na alamu zinazotoka ndani ya mwili wako, kwani hizo ni ishara za Roho Mtakatifu kukuepusha na matatizo ya dunia hii.”

“Boresha maisha ya watu kwa kadiri utakavyoweza. Ukisaidia mtu 1 watahurumiwa watu 10. Ukisaidia watu 10 watahurumiwa watu 100. Ukisaidia watu 100 watahurumiwa watu 1000. Kila mmoja wetu akitambua wajibu wake katika jamii, Mungu atatuhurumia sisi wote. Maisha ya mtu mmoja yakiboreka, mmoja huyo ataboresha na ya wengine wengi. Hivyo, endelea kuogelea lakini usisahau kurudi nyuma katika jamii.”

“Mungu humwambia mtu kitu cha kusema na mtu huwambia wenzake kile ambacho Mungu amemwambia aseme. Lakini utajuaje kama Mungu amekuchagua wewe kusema au kufanya kitu? Mungu atakwambia kupitia Roho Mtakatifu, na utajisikia msukumo mkubwa wa kusema au kufanya kile ambacho Mungu anataka useme au ufanye. Unabii unaweza kumtokea mtu yoyote, mahali popote, anayejua jinsi ya kuwasiliana na Mungu.”