Quotessence
Home / Authors / Enock Maregesi

Enock Maregesi Quotes

Author

Filter quotes by topic

Famous Enock Maregesi Quotes

“Usimwabudu mungu mwingine isipokuwa Mungu. Usimwabudu mtu, mnyama, sanamu, samaki, au usiziabudu fikira zako kichwani. Usiitumikie kazi, mali, mila, anasa, siasa, wala usiyatumikie mamlaka au usiutumikie umaarufu au ufahari, kuliko Mungu. Ukiithamini kazi, mali, mila, anasa, siasa au ukiyathamini mamlaka, au ukiuthamini umaarufu au ufahari zaidi kuliko Mungu, au ukiyapa majukumu yako muda mwingi zaidi kuliko Mungu umeabudu miungu; wakati ulipaswa kumwabudu Mungu peke yake. Usiwe na vipaumbele vingine vyovyote vile katika maisha yako zaidi ya Mungu, kwani Mungu ni Mungu mwenye wivu.”

“Heri kuishi kama maskini mwenye pesa nyingi kuliko tajiri mwenye mifuko iliyotoboka, kuliko kusema mbele za watu kwamba pesa haijakupa furaha. Wengi hupata jeuri ya kusema hivyo kutokana na umaskini wa watu wanaowazunguka.”

“Hakuna mtu mwenye akili timamu anayetaka mabaya katika maisha yake. Mwanamume atake mwanamke mwenye matendo mema. Mwanamke atake mwanamume mwenye matendo mema. Misingi ya hasanati ni misingi ya utu. Tukiishi katika misingi ya utu, misingi ya matendo mema, tutaishi sawasawa na mapenzi ya Mungu. Kila mtu anapaswa kuishi na mke au mume aliye mwema.”

“Wachawi hivi ndivyo wanavyoapishwa na kuikana imani ya Kikristo: Mwanafunzi hupelekwa kilingeni katika siku maalumu kuonana na Shetani, pamoja na jopo la wachawi. Shetani hutokea katika mwili wa hewa, mwili uliochanganyikana na hewa na mvuke mzito, wa mwanamume na kuwasihi waishikilie imani yao kwake kwa mioyo yao yote, huku akiwaahidi utajiri na maisha marefu kama hawatamkana. Kisha wachawi wanampendekeza mwanafunzi kwa Shetani. Shetani humuuliza mwanafunzi kama yuko tayari kuikana imani yake, kuachana na Ukristo na kutokumwabudu Mwanamke Aliyebarikiwa Kuliko Wanawake Wote Duniani Maria Magdalena, na kutoziheshimu sakaramenti za aina zote. Mwanafunzi atakapokubaliana na masharti hayo, Shetani atanyoosha mkono wake na kumsihi mwanafunzi anyooshe wa kwake. Kwa mkono wake mwenyewe, mwanafunzi ataapa na kuweka agano na Shetani mbele ya jopo la wachawi. Baada ya hapo bila kuchelewa Shetani ataendelea na kusema kuwa hicho kiapo hakitoshi. Lakini mwanafunzi atakapouliza afanye kitu gani cha ziada, Shetani atahitaji kiapo kifuatacho kwa heshima yake na kwa heshima ya mashetani wote: Mwanafunzi ajikabidhi kwa Shetani kwa mwili na kwa roho yake yote daima dawamu, na afanye kila awezalo kuleta wanafunzi wengine wa kike na wa kiume katika ufalme wake. Kama hiyo haitoshi Shetani ataongeza kuwa lazima mwanafunzi atengeneze mafuta fulani kutokana na mifupa na viungo vya miili ya watoto, hasa watoto waliobatizwa, kwani kwa kufanya hivyo atamtimizia kila kitu atakachokitaka hapa duniani. Hiyo ni njia mojawapo ya kiapo. Njia nyingine ya kiapo ni kwa wale ambao hawajiamini au wana hofu ya kuonana na Shetani uso kwa uso kilingeni, akiwa na mwili wa kimazingaombwe na sauti ya kutisha kwani Shetani hana mapafu wala hana ulimi. Badala ya kilingeni mwanafunzi hupelekwa kanisani na jopo la wachawi ambapo mbele ya jopo atalazimishwa kuikana imani yake, kumkana Yesu Kristo, kuukana ubatizo na kulikana kanisa zima kwa ujumla wake. Mwanafunzi baada ya hapo atalazimishwa kutoa heshima kuu kwa Mfalme Mdogo, kwani hivyo ndivyo wanavyomwita Shetani ili kumwondolea mwanafunzi hofu, kisha atalazimishwa kunywa supu ya mtoto mchanga waliyemuua akazikwa kisha wakamfukua na kupika viungo vya mwili wake; na dakika hiyo mwanafunzi atapata maarifa, maarifa ya kichawi, kama walimu wake na watarudi nyumbani.”

“Watu wa zamani katika Agano la Kale walikuwa wakiabudu miungu iliyotengenezwa kwa mawe na vinyago. Miungu hiyo haikuwa na chochote ndani mbali na kutengenezwa kwa akili na fikira za kibinadamu. Hii ilikuwa ni kinyume cha ukweli wa Kibiblia kwamba Mungu alimuumba mtu kwa mfano wake, lakini si mtu aliyejaa dhambi kumtengeneza Mungu kwa mfano wake. Kuabudu miungu mingine ni dhambi kubwa. Tii Amri Kumi za Mungu; hasa ya kwanza, ya pili na ya tatu.”

“Tupo watu takriban bilioni saba katika dunia hii. Kila mtu ni wa kipekee. Mathalani, wewe ni tofauti na baba yako au mama yako au mtu mwingine yoyote yule. Kila mtu aliumbwa kivyake na Mwenyezi Mungu. Kila mtu ana nafasi ya kwake mwenyewe aliyopangiwa na Mungu hapa duniani. Haijalishi wewe ni mwanamke au mwanamume, mweupe au mweusi, mfupi au mrefu, mzuri au mbaya, una nafasi katika nchi na dunia hii. Unachotakiwa kufanya ni kuamka, kufumbua macho na kuujua ukweli. Tafuta maarifa katika Biblia kama wewe ni Mkristo. Tafuta maarifa katika Kurani kama wewe ni Mwislamu. Tafuta maarifa katika Yoga kama wewe haumwamini Mungu. Ukishaamka na kuujua ukweli, ukishapata nafasi katika nchi yako, kuwa kiongozi na mkarimu kwa wenzako. Jifunze kutoka kwa wengine ndani na nje ya tasnia yako. Usiwe mchoyo wa maarifa. Kuwa mwadilifu. Ukifanya hivyo utafanikiwa zaidi, utaipa heshima tasnia yako, na utaacha alama katika dunia baada ya kuondoka. Kuacha alama katika dunia si lazima upate nafasi katika dunia. Kuacha alama katika dunia acha alama katika nchi yako.”

“Nyota ni kipaji, kipawa, takdiri, karama, au uweza; ni kiashiria cha rohoni kinachoonyesha mtu atakuwa nani baadaye, mafanikio ya mtu, au takdiri ya maisha ya mwanadamu. Unabii na nyota ya ufalme ni kibali cha Mungu katika maisha ya mtu. Kupata kibali hicho, tembea na watu sahihi katika maisha yako (tembea na watu ambao Mungu amekuchagulia kushika funguo za takdiri ya maisha yako). Tamka na kukiri kibali cha Mungu katika maisha yako yote. Panda mbegu za kibali cha Mungu katika udongo wa maisha yako. Jifunze kutenda mema bila malipo, kwani wema ni mbegu ya kibali cha Mungu. Jali mambo ya ufalme wa Mungu.”

“Pesa ina thamani pale unapokuwa nayo, si pale unapokuwa huna, hivyo iweke mahali unapoweza kuiona: katika nyumba, katika shamba au katika elimu. Badala ya kumpa mtu pesa ili ajenge nyumba, mpe nyumba. Badala ya kumpa mtu pesa ili afanye biashara, mpe biashara. Halafu, mpe elimu afanye maamuzi ya biashara yake. Pesa ina laana na Mungu pekee ndiye anayeweza kuiondoa laana hiyo. Ni rahisi kwa tajiri kupata baraka ya pesa kwa sababu ana pesa na ana uwezo mkubwa wa kusaidia maskini. Ni vigumu kwa maskini kupata baraka ya pesa kwa sababu hana au ana uwezo mdogo wa kusaidia maskini. Mungu anaweza kuondoa laana ya pesa kupitia hisani kwa maskini, kitu ambacho aghalabu hufanywa na matajiri wenye uwezo mkubwa. Heri kutoa kitu au huduma au elimu kwa maskini kuliko pesa.”

“Kuna vitu vitatu ndani ya mtu: kuna hiari, kuna ufahamu, na kuna mwili. Hiari inatawaliwa na Mungu; ufahamu unatawaliwa na malaika mwema; mwili unatawaliwa na nyota lakini chini ya usimamizi wa malaika wema: malaika wema walisimamisha jua na mwezi kwa ajili ya Yoshua na wana wa Israeli juu ya Gibeoni na katika bonde la Aiyaloni, walirudisha jua nyuma kwa ajili ya Hezekia mfalme wa Yuda na kwa ajili ya nabii Isaya, na waliifanya dunia ‘kuvaa koti’ ghafla wakati wa kusulubiwa kwa Mwanakondoo wa Mungu Anayeondoa Dhambi. Moyoni ni mahali patakatifu. Hata malaika wema hawawezi kuona ndani ya moyo wa mtu, ni Mungu pekee mwenye uwezo wa kufanya hivyo, na alichokihifadhi Mungu ndani ya moyo huo ni hiari ya mtu ya kuchagua mema au mabaya.”

“Mungu alimuumba mwanadamu ili aitawale dunia. Shetani tayari alikuwepo wakati Adamu anaumbwa. Adamu na Hawa walipokula tunda la mti wa katikati, walikufa kiroho – Yaani, walipoteza sura na asili ya Mungu – Shetani akawashinda kuanzia kipindi hicho na kuendelea. Tulizaliwa katika dhambi. Kila mtu anayezaliwa anazaliwa katika dhambi. Njia pekee ya kuikomboa sura na asili ya Mungu ni kumpokea Yesu (Kristo) kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako.”

“Kila mtu ana tabia, matendo, mawazo na akili yake tofauti na mtu mwingine hapa duniani. Usimdharau mtu ukidhani ana akili kama za kwako au anafikiri kama unavyofikiri wewe kwani kila mtu aliumbwa kivyake na Mwenyezi Mungu. Unaweza kudhani unamjua mtu kumbe humjui. Heshimu kila mtu kama unavyojiheshimu kwa sababu, kila mtu ni wa pekee. Kama tunavyotofautiana katika vidole na macho ndivyo tunavyotofautiana katika tabia, matendo, mawazo, imani, maadili na akili. Usimdharau mtu usiyemjua au unayedhani unamjua.”

“Maana halisi ya falsafa ya 'Nitakuwa tayari kufungwa kwa ajili ya matatizo ya watu', au Falsafa ya Kufungwa, ni uvutano mkubwa uliopo kati ya Roho Mtakatifu na Roho wa Shetani kwa sisi wanadamu wote. Jambo lolote baya limtokealo mwanadamu husababishwa na Shetani na si Mungu na watu hupata matatizo kwa sababu ya kudharau miito ya mioyo yao wenyewe, au kudharau kile Roho Mtakatifu anachowambia. Unaweza kuvunja sheria kwa manufaa ya wengi kwani mibaraka haikosi maadui. Ukifungwa kwa kuvunja sheria kwa ajili ya manufaa ya wengi watu watakulaani lakini Mungu atakubariki. Kwa nguvu ya uwezo wa Roho Mtakatifu Mungu atamshinda Shetani kwa niaba yako. Tukijifunza namna ya kuwasiliana na Roho Mtakatifu hatutapata matatizo kwani Mungu anataka tuishi kwa amani katika siku zote alizotupangia, licha ya damu yetu kuwa chafu. Mtu anapokufa kwa mfano, Roho wa Shetani amemshinda Roho Mtakatifu na Roho Mtakatifu hatalipendi hilo kwa niaba ya Mungu. Ikitokea mtu akayashinda majaribu ya Shetani katika kipindi ambacho watu wote wameyashindwa; mtu huyo amebarikiwa na Mungu, ili aitumie mibaraka hiyo kuwaepusha wenzake na roho mbaya wa Shetani. Nikisema 'Kwa nguvu ya uwezo wa Roho Mtakatifu Mungu atamshinda Shetani kwa niaba yako' namaanisha, Roho Mtakatifu ana uwezo wake na Roho wa Shetani ana uwezo wake pia. Ukimshinda Roho wa Shetani uwezo wa Roho Mtakatifu umekuwa mkubwa kuliko uwezo wa Roho wa Shetani, na ukishindwa kumtii Roho Mtakatifu uwezo wa Roho wa Shetani umekuwa mkubwa kuliko uwezo wa Roho Mtakatifu, ilhali uwezo wa Mungu ni mkubwa kuliko wa Roho Mtakatifu na wa Roho wa Shetani kwa pamoja. Mungu humtumia Roho Mtakatifu kumlindia watoto wake ambao ni sisi dhidi ya Shetani … Kila akifanyacho Roho Mtakatifu hapa duniani ni kwa niaba ya Mungu, na tukimtii Roho Mtakatifu Mungu atamshinda Shetani kwa niaba yetu. Mtu anapofungwa kwa kutetea maslahi ya umma wewe unayemfunga umemtii Roho wa Shetani. Yule anayefungwa amemtii Roho Mtakatifu maana amebarikiwa, na mibaraka haikosi maadui.”

“Badilisha tabia. Badilisha mazingira ya maisha yako. Haijalishi una umri kiasi gani au wewe ni mwanamke au mwanamume, bado hujachelewa kubadili maisha yako kutoka duni kuwa bora – kuwa na amani, furaha na kuridhika. Kama desturi yako ni kuamka saa 12:00 asubuhi kila siku ili ufike kazini saa 2:00 asubuhi ambao ni muda wa serikali wa kuanza kazi, amka saa 11:30 asubuhi ili ufike kazini saa 1:30 asubuhi – nusu saa kabla ya kuanza kazi. Kama unafanya kazi ya taaluma uliyosomea lakini maisha hayaendi, fikiria kubadili mwelekeo wa maisha ikiwemo taaluma kufikia malengo uliyojiwekea.”

“Tunazaliwa, kuteseka na kufa kwa sababu ya dhambi ya asili ya wazazi wetu wa kwanza (Adamu na Hawa). Kama Hawa asingekubali kudanganywa na Shetani, tungezaliwa bila uchungu, tungeishi bila kuteseka na tusingekufa milele. Lakini haya ndiyo mawazo yangu: Mungu Ahusiki na dhambi, Ahusiki na mwili, Anahusika na roho. Hivyo, mtu anapofariki mwili unabaki duniani lakini roho inarudi kwa Mungu; kwani Yeye ndiye aliyeitengeneza na kuiweka katika moyo wa mtu. Mimi na wewe ni viumbe vyenye thamani kubwa sana mbele za Mwenyezi Mungu; mapenzi Yake kwetu hayana masharti yoyote. Hainiingii akilini (hata kidogo) kumtesa mtu unayempenda kiasi hicho milele, wakati uwezo wa kumwokoa unao.”

“Murphy alichanganyikiwa. Hakujua nini kilitokea na kwa nini. Ila, ghafla, alipotupa macho kushoto aliona kitu. Joka kubwa lilitambaa, ingawa kwa shida, kwa sababu ya sakafu, na kumfuata kummaliza. Murphy alijua joka hata angefanya vipi, hakuwa na uwezo wa kujikinga. Alipotaka kupiga kelele ili walinzi wa nje waje, Murphy alishindwa. Nyuma ya joka – katika mkia – kuna kitu kiling’aa, kikamshangaza! Muujiza ulimtokea Murphy lakini kitu kikamwambia aite walinzi wa nje ili waje wamuue yule nyoka. Lakini kabla hajapiga kelele, alisikia sauti; si ya mwanamume. Ya mwanamke!”

“Watoto wadogo wanakufa. Watu wazima wasiokuwa na hatia wanakufa vitani na katika majanga mengine ya asili. Kwa nini? Watoto wadogo wanaokufa walikuja duniani kufanya nini? Kwa nini watu wasiokuwa na hatia wanakufa ilhali Mungu yupo na asiwaepushe na matatizo ya dunia hii? Kama aliweza kuzuia binadamu wasiishi majini kwa sababu watakufa kwa nini asizuie matatizo yasiwapate watoto na watu wazima wasiokuwa na hatia? Sisi ni wadogo sana na Mungu ni mkubwa mno. Jibu hatutaweza kulielewa pamoja na kwamba tumepewa. Hata hivyo, Mungu hababaishwi na mwili. Anababaishwa na roho.”

“Mwili wako una uwezo wa kujua kabla yako kitakachotokea baadaye. Kama una njaa kwa mfano, mwili wako utakwambia. Kama una kiu, mwili wako utakwambia. Kama unaumwa, mwili wako utakwambia. Kama kuna kitu kibaya kinatarajia kutokea katika maisha yako au katika maisha ya mtu mwingine, mwili wako utakwambia. Kuwa makini na alamu zinazotoka ndani ya mwili wako, kwani hizo ni ishara za Roho Mtakatifu kukuepusha na matatizo ya dunia hii.”

“Mungu humwambia mtu kitu cha kusema na mtu huwambia wenzake kile ambacho Mungu amemwambia aseme. Lakini utajuaje kama Mungu amekuchagua wewe kusema au kufanya kitu? Mungu atakwambia kupitia Roho Mtakatifu, na utajisikia msukumo mkubwa wa kusema au kufanya kile ambacho Mungu anataka useme au ufanye. Unabii unaweza kumtokea mtu yoyote, mahali popote, anayejua jinsi ya kuwasiliana na Mungu.”