Quotessence
Home / Authors / Enock Maregesi

Enock Maregesi Quotes

Author

Filter quotes by topic

Famous Enock Maregesi Quotes

“Sina jinsi. Nguzo ya maisha yangu ni historia ya maisha yangu. Historia ya maisha yangu ni urithi wa watu waliojifunza kusema hapana kwa ndiyo nyingi – waliojitolea vitu vingi katika maisha yao kunifikisha hapa nilipo leo – walionifundisha falsafa ya kushindwa si hiari. Siri ya mafanikio yangu ni kujitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu wote; au 'pushing the envelope' kwa lugha ya kigeni.”

“Mungu hutumia watu 'wajinga' na 'wapumbavu' kufanya mambo makubwa katika maisha yao na ya watu wengine. Katika Biblia, Musa aliitwa mjinga alipokiuka amri ya Farao ya kuendelea kuwafanya watumwa wana wa Israeli nchini Misri; Nuhu aliitwa mpumbavu alipohubiri kwa miaka mia kuhusu gharika, katika kipindi ambacho watu hawakujua mvua ni nini; Daudi aliitwa mjinga alipojitolea kupambana na Goliati bonge la mtu, shujaa wa Gathi; Yusufu aliitwa mjinga alipokataa kulala na mke wa bosi wake, baada ya kuwa ameuzwa na nduguze kama mtumwa nchini Misri; Abrahamu aliitwa mjinga alipoamua kuhama nchi aliyoipenda na kwenda katika nchi ya ahadi, eti kwa sababu Mungu alimwambia kufanya hivyo; Yesu aliitwa mjinga mpaka akasulubiwa aliposema yeye ni Mfalme na Mwana wa Mungu. LAKINI, Musa alitenganisha Bahari ya Shamu na kuwapeleka Waisraeli katika nchi ya ahadi, ambako aliwakomboa kutoka utumwani. Nuhu aliokoa dunia. Daudi alimshinda Goliati. Yusufu aliokoa familia yake kutokana na njaa. Abrahamu alikuwa baba wa imani. Yesu aliyashinda mauti. Wakati mwingine tunatakiwa kufanya mambo makubwa kulingana na jinsi Roho Mtakatifu anavyotutuma, bila kujali watu au dunia itasemaje.”

“Nyota ni kipaji, kipawa, takdiri, karama, au uweza; ni kiashiria cha rohoni kinachoonyesha mtu atakuwa nani baadaye, mafanikio ya mtu, au takdiri ya maisha ya mwanadamu. Unabii na nyota ya ufalme ni kibali cha Mungu katika maisha ya mtu. Kupata kibali hicho, tembea na watu sahihi katika maisha yako (tembea na watu ambao Mungu amekuchagulia kushika funguo za takdiri ya maisha yako). Tamka na kukiri kibali cha Mungu katika maisha yako yote. Panda mbegu za kibali cha Mungu katika udongo wa maisha yako. Jifunze kutenda mema bila malipo, kwani wema ni mbegu ya kibali cha Mungu. Jali mambo ya ufalme wa Mungu.”

“Aidha, tunaweza kupata inkishafi kutokana na asili ya miili yetu, matukio fulani ya wakati ujao yana asili yake katika ndoto za binadamu. Ndoto hizo au maono hayo ni ishara ya kile kinachokuja mbele katika maisha ya mtu; kama vile afya, ugonjwa au hatari. Ukiota kuhusu moto, hiyo ni ishara ya hasira – unatakiwa kuwa na hekima; ukiota kuhusu mimba na unajifungua, hiyo ni ishara ya kuwa katika mchakato wa kutengeneza wazo jipya – unatakiwa kushukuru; ukiota unaruka angani, hiyo ni ishara ya tumaini – unatakiwa kushukuru; ukiota kuhusu maji au kiowevu kingine chochote kile, hiyo ni ishara ya siri na wakati mwingine ni ishara ya kuwa na matatizo ya kiafya kama utaota kuhusu maji machafu – unatakiwa kuwa msiri na msafi; ukiota kuhusu ardhi, hiyo ni ishara ya huzuni – unatakiwa kuomba; na ukiota kuhusu Yesu, hiyo ni ishara ya mafanikio – unatakiwa kushukuru.”

“Ukifuata kanuni ya nguvu ya uvutano uhitaji kujua jinsi utakavyofanikiwa. Kazi yako ni kuwaza tu kwa namna inavyotakiwa. Waza na amini kwa asilimia mia moja. Mengine yote mwachie Mungu au ulimwengu. Mungu pekee ndiye anayekupa njia na bahati, ili wewe ufanikiwe. Atakupa nguvu ya kufanya kazi na ujanja wowote utakaohitajika, katika harakati hizo za mafanikio yako.”

“Siri ya mafanikio yako ni chumba chako. Dali linasema anga ndicho kipimo cha kufikiria; Dirisha linasema utazame nje uone fursa zilizopo ulimwenguni; Feni linasema uwe mtulivu usikurupuke kufanya lolote; Kalenda inasema uwe mtu anayekwenda na wakati; Kioo kinasema ujitazame na ujiamini kabla ya kutenda lolote; Kitabu cha dini kinasema unapaswa kumwamini Mungu ili uishi; Kitanda kinasema ujifunze kuwa na likizo; Mlango unasema usipitwe na fursa ya aina yoyote ile hapa duniani; Saa inasema kila sekunde ina thamani sana katika maisha yako hivyo tumia muda wako vizuri. Amka uishi.”

“Damu ya Mwanakondoo ina nguvu kuliko maombi. Mungu hauwi, Anamtumia Shetani kama wakala wake wa kutoa adhabu kwa binadamu. Ukifunikwa na damu ya Mwanakondoo Shetani, ambaye ni wakala, hatakuona. Lakini Mungu atakuona. Bila kafara ya damu hakuna msamaha wa dhambi. Bila kafara ya damu hakuna mafanikio.”

“Kuna ndoto za mchana na kuna ndoto za usiku. Ndoto za mchana ni maono ya kile ambacho roho inatamani kuwa. Ndoto za usiku ni maono yanayotokea wakati akili imetulia baada ya mwili wote kupumzika. Ukiota kuhusu moto, hiyo ni ishara ya hasira; ukiota kuhusu maji, hiyo ni ishara ya siri; ukiota kuhusu ardhi, hiyo ni ishara ya huzuni; ukiota kuhusu Yesu, hiyo ni ishara ya mafanikio. Kitu cha kwanza kufanya unapoota ndoto za kishetani, utakapoamka, mwombe Mungu akunusuru kutoka katika matatizo yoyote yanayokunyemelea; au yanayomnyemelea mtu mwingine yoyote yule, hata usiyemjua. Ubongo ni kitu cha ajabu kuliko vyote ulimwenguni na umetengenezwa na Mungu. Ndoto zinapatikana ndani ya ubongo. Ubongo unapatikana ndani ya ufahamu. Ufahamu mtawala wake ni malaika mwema. Malaika mwema anajua siri ya ndoto. Kila mtu anaota na kila ndoto ina maana yake. Rekodi ndoto zako kila siku kwa angalau mwezi mzima kupata maana halisi ya ndoto hizo, na kujua kwa nini ulizaliwa.”

“Mungu akikubariki kipaji chako watu watasema ni laana. Maisha yako ni sawa na mto. Unakoelekea ni baharini. Lakini sasa umefika kwenye mlango wa bahari. Unahangaika upite wapi kufika baharini, ambapo utaogelea kwa kadiri utakavyoweza. Utakapofika baharini, watu, badala ya kusema umebarikiwa, watasema umelaaniwa, badala ya kukuita malaika, watakuita shetani. Mafanikio hayapimwi kwa pesa au mali kiasi gani unayo, mafanikio yanapimwa kwa amani ya moyo au maisha ya watu kiasi gani umeboresha.”

“Ukiwaza kwa kufuata kanuni ya nguvu ya uvutano (ambayo ni kuwaza na kuamini kama kile unachokiwaza tayari umeshakipata bila hata kujua umekipataje) utaishi kama ulivyowaza. Ukiwaza kuwa jambazi utakuwa jambazi hakika, ukiwaza kupona ugonjwa unaokusumbua utapona hakika, na ukiwaza kuwa tajiri utakuwa tajiri hakika. Mafanikio hayo yanaweza kuchukua mwezi mmoja kutimia au yanaweza kuchukua miaka kumi. Unachotakiwa kufanya ni kuwaza na kuamini.”

“Kufanikiwa katika maisha lazima kitu fulani ambacho si cha kawaida kitokee katika maisha yako, bila kujali uko upande wa Yesu au upande wa Shetani. Kufanikiwa katika maisha ni sawa na kwenda mbinguni, au kuishi mbinguni duniani. Kitu ambacho si cha kawaida kutokea katika maisha yako ni sawa na kifo. Fanya kitu ambacho hujawahi kufanya kupata kitu ambacho hujawahi kupata.”

“Kufika hapa nilipofika leo nilijitolea vitu vingi na mambo mengi katika maisha yangu. Niliishi katika uhamisho wa kijamii kwa ajili ya mafanikio. Nilijitolea muda. Nilijitolea usingizi. Nilijitolea starehe. Wakati wengine wakienda baa mimi nilikuwa kazini. Wakati wengine wamelala, mimi nilikuwa macho nikifanya kazi. Wakati wengine wakiangalia vipindi pendwa vya televisheni, mimi nilikuwa nikiangalia vipindi visivyopendeka vya televisheni. Wakati wengine wana muda wa kuchezea, mimi nilikuwa nikiyaendesha maisha yangu kwa ratiba maalumu.”