Quotessence
Home / Authors / Enock Maregesi

Enock Maregesi Quotes

Author

Filter quotes by topic

Famous Enock Maregesi Quotes

“Askari wa Kirumi alimchoma Yesu mkuki ili andiko litimie. Askari huyo ambaye Biblia haikumtaja jina kwa sababu zilizoko nje ya uwezo wetu, alivyoona kweli amepona na ameona alishuhudia, na ushuhuda wake ulitoka moyoni, ili nasi tupate kusadiki. Wauaji wa Kirumi walipoona kwamba wale wezi waliosulubiwa pamoja na Yesu walikuwa bado hawajakata roho, waliwavunja miguu ili washindwe kupumua na hivyo kuharakisha kifo chao. Kwa upande wa Yesu, waliona alishapoteza fahamu na labda alishafariki. Kuthibitisha hilo askari wa Kirumi alirusha mkuki, nao ukatoboa utando unaozunguka moyo wa Yesu na mapafu ya Yesu, na damu na maji kutoka. Lakini yote hayo yalishatabiriwa miaka mingi kabla ya Yesu: ‘Hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa’ na ‘Nao watamtazama yeye ambaye walimchoma’.”

“Wanasayansi wanaamini kuwa Yesu atarudi tarehe 29 Julai 2016. Tarehe hiyo kitu kikubwa sana kitatokea katika dunia yetu kitakachosababisha tetemeko kubwa la ardhi, litakalosababishwa na kubadilika kwa ncha za dunia, tendo litakalosababisha mionzi ya gama kutoka kwenye jua ifike duniani na kuua kila kitu kinachoonekana katika uso wa dunia hii. Watakatifu watafufuka na kumlaki Kristo mawinguni, ambaye anakuja kuwachukua wateule na kumweka Shetani kifungoni kwa miaka 1000. Hayo yote, wanasema, yatatokea ndani ya siku 11 kuanzia leo. Yaani, kusini mwa dunia kutakuwa kaskazini mwa dunia, kaskazini mwa dunia kutakuwa kusini mwa dunia. Kitendo hicho kitafanya dunia ikose kinga ya sumaku iitwayo ‘magnetosphere’ ambayo hukinga dunia dhidi ya mionzi ya gama kutoka kwenye jua. Mionzi hiyo hugonga ukuta wa ‘magnetosphere’ kila baada ya dakika 8 kwa mwendokasi wa kilometa milioni 1080 kwa saa; na kusambazwa katika ncha za dunia ambapo aghalabu huchanganyikana na oksijeni na kutengeneza kitu kinaitwa ‘aurora’, au mwanga wa ncha, ambacho ni maajabu mengine ya angani. Mwaka 2012 wanasayansi walisema ncha za dunia zingebadilika lakini hazikubadilika. Je, muda umefika sasa wa kuwaamini wanasayansi? Biblia ni chuo cha Mungu. Soma Biblia kupata maarifa.”

“Biblia inatuambia kuwa tuombe bila kukoma. Lakini tutaombaje bila kukoma? Njia mojawapo ya kufanya hivyo ni kutumia ‘maombi ya pumzi’ kila siku kama ambavyo Wakristo wengi wamekuwa wakifanya kwa karne nyingi. Unachagua sentensi fupi au maneno rahisi kuhusu Yesu unayoweza kuyasema na kuyarudia kimoyomoyo kila siku katika kila pumzi inayoingia na kutoka ndani ya mapafu yako! Kwa mfano: “Asante Yesu.” “U pamoja nami.” “Nataka kukujua.” “Napokea neema yako.” “Nakutegemea wewe.” “Mimi ni wako.” “Nisaidie nikuamini.” “U Mungu wangu.” “Naishi kwa ajili yako.” “Nisamehe dhambi zangu zote.” Fundisha akili yako kumkumbuka Mungu kila wakati.”

“Mitume kumi na wawili wa Yesu Kristo waliamua kufa kinyama kulinda heshima ya mfalme wao Yesu Kristo, kama Biblia na historia vinavyosema. Kwa nini watu (wengine) wa kizazi hiki wanasema hakuna Mungu na kwa sababu hiyo hawamwamini Yesu? Je, uko tayari kufa kwa ajili ya mtu aliyekufa kwa ajili yako? Kwa ajili ya mtu ambaye mitume walikuwa tayari kufa kwa ajili yake? Je, wewe una akili zaidi kuliko mitume? Yesu aliamua kufa ili wewe uishi, lakini bado unakuwa mbishi. Badilika.”

“Mungu hutumia watu 'wajinga' na 'wapumbavu' kufanya mambo makubwa katika maisha yao na ya watu wengine. Katika Biblia, Musa aliitwa mjinga alipokiuka amri ya Farao ya kuendelea kuwafanya watumwa wana wa Israeli nchini Misri; Nuhu aliitwa mpumbavu alipohubiri kwa miaka mia kuhusu gharika, katika kipindi ambacho watu hawakujua mvua ni nini; Daudi aliitwa mjinga alipojitolea kupambana na Goliati bonge la mtu, shujaa wa Gathi; Yusufu aliitwa mjinga alipokataa kulala na mke wa bosi wake, baada ya kuwa ameuzwa na nduguze kama mtumwa nchini Misri; Abrahamu aliitwa mjinga alipoamua kuhama nchi aliyoipenda na kwenda katika nchi ya ahadi, eti kwa sababu Mungu alimwambia kufanya hivyo; Yesu aliitwa mjinga mpaka akasulubiwa aliposema yeye ni Mfalme na Mwana wa Mungu. LAKINI, Musa alitenganisha Bahari ya Shamu na kuwapeleka Waisraeli katika nchi ya ahadi, ambako aliwakomboa kutoka utumwani. Nuhu aliokoa dunia. Daudi alimshinda Goliati. Yusufu aliokoa familia yake kutokana na njaa. Abrahamu alikuwa baba wa imani. Yesu aliyashinda mauti. Wakati mwingine tunatakiwa kufanya mambo makubwa kulingana na jinsi Roho Mtakatifu anavyotutuma, bila kujali watu au dunia itasemaje.”

“Ukipata matatizo kumbuka kwamba Yesu alipata matatizo pia, na kutokana na matatizo hayo mimi na wewe tulipata uhuru. Soma Biblia. Soma nyimbo katika kitabu cha Zaburi zinazomsifu Mungu katika kipindi cha matatizo. Funga na kuomba ukiamini kwamba mapenzi ya Mungu kwetu ni huru, yasiyokuwa na masharti yoyote. Toa msamaha kwa waliokukosea. Ni kitu cha muhimu kujilimbikizia imani katika kipindi cha amani, ili matatizo yakitokea usiweze kuyumba.”

“Mungu alimuumba mwanadamu ili aitawale dunia. Shetani tayari alikuwepo wakati Adamu anaumbwa. Adamu na Hawa walipokula tunda la mti wa katikati, walikufa kiroho – Yaani, walipoteza sura na asili ya Mungu – Shetani akawashinda kuanzia kipindi hicho na kuendelea. Tulizaliwa katika dhambi. Kila mtu anayezaliwa anazaliwa katika dhambi. Njia pekee ya kuikomboa sura na asili ya Mungu ni kumpokea Yesu (Kristo) kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako.”

“Mfalme Sulemani alikuwa mtu mwenye hekima kuliko wote ulimwenguni. Anatushauri, “Adui yako akiwa ana njaa, mpe chakula; Tena akiwa ana kiu, mpe maji ya kunywa; Maana utatia makaa ya moto kichwani pake; Na BWANA atakupa thawabu (Mithali 25:21-22). Yesu anasema jambo fulani linalofanana sana na hilo katika mafundisho Yake yaliyofuata (Mathayo 5:44-45). Kitendo cha kutukanwa, kupigwa, kushtakiwa au kulazimishwa kubeba mzigo mzito usio wa kwako kinaweza kusababisha mafutu mabaya kabisa katika asili ya binadamu. Yaani, chuki, hasira, ukatili na hata vurugu. Lakini pale wale waliobarikiwa kuwa na hekima wanapojikuta katika majaribu makubwa kama hayo tabia yao haitakiwi kuwa ya shari, inda au ya kulipiza kisasi. Bali inatakiwa kuwa ya kusaidia, kuwa na ridhaa ya kutenda mambo mema, na kuwa mwema kwa wengine siku zote.”

“Msamaha si jambo dogo. Watu wadogo, watu wenye uwezo mdogo wa kufikiri, hawawezi kupambana na changamoto za msamaha. Msamaha ni kwa ajili ya watu wenye macho kama ya tai wanaoweza kuona mbali ambao wako tayari kushindwa vita ili washinde vita. Hewa inaingia ndani ya mapafu na kutoka; chakula kinaingia ndani ya mwili na kutoka; mwanamasumbwi anapigana bila kugombana; injini ya gari haiwezi kusukuma gari mbele au nyuma bila kutoa hewa katika paipu ya ekzosi. Lakini kile kinachoingia moyoni mwako hakitoki! Maumivu yanapoingia ndani ya moyo yanapaswa kutoka nje kama yalivyoingia kwa sababu, yasipotoka yatatengeneza sumu ndani ya moyo wako na yatatengeneza sumu ndani ya roho yako pia. Sumu hiyo itahatarisha safari yako ya mbinguni na Mungu hatakusamehe tena. Badala ya yule aliyekukosea kuumia, utaumia wewe uliyekosewa. Yesu anaposema samehe saba mara sabini hatanii. Usiposamehe, hutasamehewa.”

“Aidha, tunaweza kupata inkishafi kutokana na asili ya miili yetu, matukio fulani ya wakati ujao yana asili yake katika ndoto za binadamu. Ndoto hizo au maono hayo ni ishara ya kile kinachokuja mbele katika maisha ya mtu; kama vile afya, ugonjwa au hatari. Ukiota kuhusu moto, hiyo ni ishara ya hasira – unatakiwa kuwa na hekima; ukiota kuhusu mimba na unajifungua, hiyo ni ishara ya kuwa katika mchakato wa kutengeneza wazo jipya – unatakiwa kushukuru; ukiota unaruka angani, hiyo ni ishara ya tumaini – unatakiwa kushukuru; ukiota kuhusu maji au kiowevu kingine chochote kile, hiyo ni ishara ya siri na wakati mwingine ni ishara ya kuwa na matatizo ya kiafya kama utaota kuhusu maji machafu – unatakiwa kuwa msiri na msafi; ukiota kuhusu ardhi, hiyo ni ishara ya huzuni – unatakiwa kuomba; na ukiota kuhusu Yesu, hiyo ni ishara ya mafanikio – unatakiwa kushukuru.”

“Kilio kikuu cha Yesu, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?”, yaani, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”, na “Imekwisha”, vilitabiriwa katika Zaburi 22 ili watu waliompinga Kristo waamini kama Yesu alikuwa Masihi. Zaburi 22 ulikuwa wimbo maarufu katika kipindi cha karne ya kwanza, kipindi ambacho Yesu alizaliwa na kufa, uliotungwa na mfalme Daudi, ulioitwa ‘zaburi ya mateso na matumaini ya mwadilifu’. Kwa hiyo Yesu aliposema maneno hayo yaliwaingia watu akilini, na kuanzia hapo imani hasa ya Ukristo ikachukua kasi hadi leo hii. Zaburi 22 inaanza na “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” na inaisha na “Imekwisha”, miongoni mwa maneno saba aliyoyasema Yesu pale msalabani Golgotha. Kwa hiyo, Zaburi 22 ni utabiri wa kifo cha Yesu.”

“Yesu alikuwa binadamu ili afe kama binadamu kwa ajili ya binadamu. Alikufa msalabani ili sisi wote tuokoke. Lakini Shetani hataki hilo litokee. Akiingilia uumbaji wa Mungu toka tumboni mwa binadamu, binadamu atakayezaliwa hatakuwa na uwezo wa kuongoka. Atakuwa na roho ya jini itakayomjua Shetani badala ya kumjua Mungu. Hivyo kurudi kwa Yesu kwa mara ya pili hakutakuwa na maana, kwa sababu hakutakuwepo na mtu wa kuokolewa.”

“Shetani na wafuasi wake wako kifungoni sasa hivi kwa sababu dhambi walizotenda hazisameheki. Dhambi ya kumkana Mungu na kumkubali Shetani haisameheki. Kwa maana nyingine, ukimuuzia Shetani roho yako jina lako halitaandikwa katika kitabu cha uzima litaandikwa katika kitabu cha mauti. Ukibidika kuuza roho, usimuuzie Shetani, muuzie Yesu.”

“Kuna ndoto za mchana na kuna ndoto za usiku. Ndoto za mchana ni maono ya kile ambacho roho inatamani kuwa. Ndoto za usiku ni maono yanayotokea wakati akili imetulia baada ya mwili wote kupumzika. Ukiota kuhusu moto, hiyo ni ishara ya hasira; ukiota kuhusu maji, hiyo ni ishara ya siri; ukiota kuhusu ardhi, hiyo ni ishara ya huzuni; ukiota kuhusu Yesu, hiyo ni ishara ya mafanikio. Kitu cha kwanza kufanya unapoota ndoto za kishetani, utakapoamka, mwombe Mungu akunusuru kutoka katika matatizo yoyote yanayokunyemelea; au yanayomnyemelea mtu mwingine yoyote yule, hata usiyemjua. Ubongo ni kitu cha ajabu kuliko vyote ulimwenguni na umetengenezwa na Mungu. Ndoto zinapatikana ndani ya ubongo. Ubongo unapatikana ndani ya ufahamu. Ufahamu mtawala wake ni malaika mwema. Malaika mwema anajua siri ya ndoto. Kila mtu anaota na kila ndoto ina maana yake. Rekodi ndoto zako kila siku kwa angalau mwezi mzima kupata maana halisi ya ndoto hizo, na kujua kwa nini ulizaliwa.”

“Ufalme wa mbinguni uko juu. Akili ya binadamu iko juu. Kupata Amri Kumi za Mungu, Musa alipanda juu katika mlima Sinai. Yesu alijaribiwa na Shetani akiwa juu katika jangwa la Yuda. Ukifanikiwa tunasema uko juu. Tai hawezi kuona vizuri akiwa chini anaweza kuona vizuri akiwa juu. Ulaya na Amerika tunaita majuu kwa sababu ziko juu ya ikweta. Kwa nini juu? Kwa sababu juu kuna utukufu.”

“Kuna ushahidi wa kutosha katika maandiko kwamba Yesu aliugua hipovolimia kutokana na kuchapwa. Yesu alipobeba msalaba wake kuelekea Golgotha alianguka, na mtu mmoja aliyeitwa Simoni alilazimishwa ama kuubeba au kumsaidia Yesu kuubeba msalaba huo hadi kilimani. Kuanguka huko kunaonyesha kwamba Yesu alikuwa na shinikizo la damu. Alama nyingine inayoonyesha kwamba Yesu alipatwa na ugonjwa wa hipovolimia ni pale alipodai kuwa alikuwa na kiu, akiwa msalabani, akimaanisha kiu ya maji.”

“Kabla ya kukata roho mapigo ya kasi ya moyo aliyoyapata Yesu kutokana na mshtuko wa hipovolimia, pia yalisababisha maji kujikusanya katika vifuko vya maji au ute kandokando ya moyo na kandokando ya mapafu. Mkusanyiko huu wa maji kandokando ya moyo hujulikana kama ‘pericardial effusion’ na mkusanyiko wa maji kandokando ya mapafu hujulikana kama ‘pleural effusion’. Hii ndiyo maana baada ya Yesu kukata roho, na askari wa Kirumi kurusha mkuki katika ubavu wake, baada ya kutoboa mapafu na moyo, damu na maji vilitoka katika mbavu za Yesu kama Yohana alivyorekodi katika Injili yake. Mapafu ya Yesu na tumbo la Yesu vilijaa damu na maji. Mkuki ulivyotupwa maji yalitoka katika mapafu ya Yesu na katika tumbo la Yesu, na katika utando unaozunguka moyo wa Yesu, kutokana na kupasuka kwa moyo.”

“Unaweza kuwa umeomba kuhusu jambo fulani kwa muda mrefu bila majibu, lakini siku moja ghafla ukajibiwa wakati umejisahau. Kwa nini? Kwa sababu Mungu hufanya kazi zake kwa siri. Ukiomba jambo kutoka kwa Mungu, huku ukiwa huna kinyongo na mtu yeyote na bila moyo wako kusita wakati ukiomba, tambua katika moyo wako kwamba tayari umeshajibiwa. Kisha lipotezee, hilo jambo, kila siku, usiwe unalikumbukakumbuka, hadi Mungu mwenyewe atakapokujibu. Hata Yesu atakaporudi kila mtu atakuwa amejisahau.”

“Hakimu na Kuhani Mkuu wa Shilo Eli alipata matatizo makubwa wakati wa mgogoro wa Waisraeli na Wafilisti, kati ya mwaka 2871 na 2870 Kabla ya Kristo. Mara tu baada ya kupewa taarifa ya kifo cha watoto wake wawili, Hofni na Finehasi, na kutwaliwa kwa Sanduku la Agano la Bwana wa Majeshi lililohifadhi Amri Kumi za Mungu, Eli alianguka kutoka katika kiti chake na kufariki papo hapo akiwa na umri wa miaka 98. Aidha, mkwe wa Eli, mke wa Finehasi, alijifungua ghafla na kufariki alipopata taarifa ya kifo cha mkwewe na taarifa ya kuuwawa kwa mumewe na ya kutekwa nyara kwa Sanduku la Agano. Mwanajeshi kutoka Benyamini falaula angetumia hekima na busara kutoa taarifa ya kifo na ya kutwaliwa kwa Sanduku la Agano huenda Eli asingefariki, na huenda mkwewe asingejifungua mtoto njiti na huenda asingekufa siku hiyo. Kwani Sanduku la Agano lilirejeshwa nchini Israeli, na Wafilisti wenyewe, baada ya miezi saba tangu litwaliwe, na kifo cha watoto wa Eli yalikuwa mapenzi ya Mungu. Hivyo Eli asingeweza kuzuia kifo cha watoto wake, na Wafilisti wasingeweza kukaa na Sanduku la Agano milele. Lakini katika kafara ya Isaka ambapo Isaka aliamua kujitoa kafara mwenyewe kumfurahisha Mungu na baba yake kama Yesu alivyoamua kujitoa kafara mwenyewe kumfurahisha Mungu na baba yake wa mbinguni, Sara angekufa kama Ibrahimu hangetumia hekima alipomwambia anakwenda kumtolea Bwana kafara ya mwanakondoo wakati akijua anakwenda kumtoa Isaka mtoto wa pekee wa Sara. Hekima inatoka moyoni, busara inatoka mdomoni. Kwa vile suala la kutoa taarifa mbaya kwa mtu ni gumu kwa yule anayetoa na kwa yule anayepokea, hekima na busara havina budi kutumika.”

“Taabini hii ni ngumu sana kwangu kuandika pamoja na kwamba ni miaka mitatu kamili toka giza liingie. Mwaka 2014, Novemba 4, nilimpoteza bibi yangu mpendwa, Martha Maregesi, aliyefariki dunia kutokana na ukongo wa kiharusi, na tutamkumbuka daima. Alikuwa na roho ya kipekee; na kifo chake kiliwagusa wengi, pamoja na kwamba aliishi maisha kamili, zaidi ya siku 25550, siku 5110 zaidi, ambazo ndizo tulizopangiwa na Mungu. Mapenzi ya mtu kwa bibi yake ni mapenzi ya kipekee. Nadhani Mungu aliwapa mabibi wote uwezo maalumu wa kuwapenda wajukuu zao, na kufanya maisha yao yatimie, kuwafanya wawe binadamu wazuri na wenye maadili mema. Alichangia pakubwa katika malezi yangu ya utotoni; na aghalabu naweza kukumbuka nikiwa naye jikoni akipika, huku mimi nikifanya kazi nyingine, lakini wakati huohuo akinifundisha mambo kadha wa kadha ya kunikomaza kimaisha. Bibi hakuwa tu bibi. Alikuwa mlezi, rafiki na mtu aliyenihamasisha sana katika maisha. Kifo kinaleta huzuni lakini kinaleta tumaini. Naamini bibi yangu atakwenda mbinguni, kwa sababu naamini alitubu dhambi zake akisaidiwa na wachungaji. Wachungaji hao walimtembelea kila siku, nyumbani au hospitalini, akiwa kitandani kwake akiugua. Bibi yangu alitimiza wajibu wake. Alizaliwa, aliishi, na alikufa katika toba. Siku nitakapokufa ningependa kuzikwa jirani na alipozikwa bibi yangu, ili Yesu atakaporudi tufufuke pamoja.”

“Watakatifu wote watanyanyuliwa na wataondoka pamoja na Yesu kuelekea mbinguni, kwa ajili ya ziara ya miaka 1000 katika ulimwengu wa roho; kuanzia dunia ya kwanza ya ulimwengu huo iitwayo Asiyah hadi ya mwisho iitwayo Adam Kadmon, katika mji mpya wa Yerusalemu. Baada ya milenia, kipindi hicho huku duniani Ibilisi akiwa kifungoni na malaika wake, binadamu wote wenye dhambi wakiwa wamekufa, Yesu na watakatifu wote atarudi kwa ajili ya ufufuo wa pili; na kama mfalme wa ulimwengu wote milele.”

“Yesu alipokuwa msalabani watu wengi walimzunguka. Askari wa Kirumi aliyekuwa na chongo, na mkuki, alikuwa na jukumu la kumtesa Yesu hadi kufa kwa amri ya Pilato. Yesu alipolia kwa sauti kuu, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?”, yule askari alikurupuka na kumwendea Yesu. Lakini Yesu alishakata roho. Kuthibitisha kama Yesu alishakata roho, askari alimchoma Yesu mkuki kwenye mbavu kwa nguvu zake zote. Mkuki huo ukamtoboa Yesu hadi upande wa pili, ukatoboa hata moyo wake. Askari alipochomoa mkuki, damu na maji viliruka na kupiga jicho lake bovu. Papo hapo askari akapona na kuona vizuri. Alipoona kweli amepona na kuona vizuri, askari alipiga kelele, alipiga magoti na kuomba Mungu amsamehe dhambi zake. Msamaha una nguvu kuliko dhambi. Askari huyo atakwenda mbinguni. Haijalishi umechukia watu kiasi gani. Haijalishi umetesa watu kiasi gani. Haijalishi umeua watu kiasi gani. Haijalishi umetenda dhambi kiasi gani. Mungu anachotaka kutoka kwako, tubu.”

“Utajiri wa mbinguni ni wa milele na mungu wake ni Yehova. Utajiri wa duniani ni wa muda na mungu wake ni Mammon. Mammon, ambaye hata Yesu alimtaja katika Injili ya Mathayo 6 na katika Injili ya Luka 16, ni mungu wa uchoyo na utajiri wa dunia hii. Mammon kazi yake ni kufanya watu waliokufa kifedha na walio hai kifedha kuwa maskini wa milele ahera. Yesu Kristo alikuwa maskini, ili tuwe matajiri kupitia umaskini wake, lakini kwa sababu alikuwa na imani ya Mungu katika moyo wake alikuwa tajiri. Hivyo unaweza kuwa na utajiri wa mbinguni hapa duniani, ukiikaribisha amani ya Mungu katika moyo wako.”

“Kufanikiwa katika maisha lazima kitu fulani ambacho si cha kawaida kitokee katika maisha yako, bila kujali uko upande wa Yesu au upande wa Shetani. Kufanikiwa katika maisha ni sawa na kwenda mbinguni, au kuishi mbinguni duniani. Kitu ambacho si cha kawaida kutokea katika maisha yako ni sawa na kifo. Fanya kitu ambacho hujawahi kufanya kupata kitu ambacho hujawahi kupata.”