Quotessence
Home / Authors / Enock Maregesi

Enock Maregesi Quotes

Author

Filter quotes by topic

Famous Enock Maregesi Quotes

“Bibi Martha Maregesi aliishi maisha mazuri sana hapa duniani. Alibarikiwa na Mungu. Aliishi miaka 84 – siku 30660 badala ya siku 25550 tulizopangiwa na Mungu. Katika uhai wake wote, kwa wale wote aliowalea, hakuna mtoto wake hata mmoja aliyefariki kabla yake. Hakuna mjukuu wake hata mmoja aliyefariki kabla yake. Hakuna kitukuu chake hata kimoja kilichofariki kabla yake. Bibi yangu ametimiza mwaka mmoja kamili leo hii, tangu amefariki dunia Novemba 4 mwaka 2014 mjini Musoma. Tunamkumbuka leo akiwa amefariki kama tulivyomkumbuka jana akiwa hai. Nguvu ya sala zetu imfanye Mwenyezi Mungu aendelee kumsamehe dhambi zake zote, na amweke mahali anapostahili, Amina.”

“Ukiua mtu bila kumwambia kwa nini unamuua anaweza kujua umemuua kwa kumwonea. Akijua umemuua kwa kumwonea roho yake inaweza kukusumbua wewe na familia yako maisha yenu yote. Makachero wa EAC wana leseni ya kuua. Lakini si kuua ovyo kama James Bond. Kila wanayemuua lazima waandike ripoti kwa nini wamemuua. Kachero wa EAC akiua mtu, kwa makosa, kwa bahati mbaya, atalindwa na Mwenyezi Mungu. Atalindwa na Tambiko la Tume ya Dunia.”

“Kujua nini kitatokea kesho, au kesho kutwa, au kujua jinsi usaili wako wa kazi utakavyokuwa, au ni maswali gani utakayoulizwa kwenye mtihani kwa mfano, kutarahisisha sana maisha yetu. 'Madirisha' madogo katika kipindi cha saa za usoni hufunguka mara kwa mara katika maisha yetu, kimiujiza na bila kutegemea. Hudokeza kidogo jinsi tukio fulani, au hali fulani, au kitu fulani kitakavyotokea katika kipindi cha wakati ujao bila sisi wenyewe kujua. Hali hii hujulikana kama jakamoyo. Jakamoyo ni sanaa ya kubashiri vitu visivyojulikana. Kazi yake ni kutuhadharisha na kutusaidia! Kujua mapema hatari iliyoko mbele yako inamaanisha kuwa na uwezo wa kujilinda kutokana na hatari hiyo, na kuwa na uwezo wa kuepuka mitego. Jakamoyo huweza kumtokea mtu katika hali ya 'maono', au 'mwako wa mwanga' (yaani kufumba na kufumbua). Mara nyingi huonekana kama ndoto. Hutokea wakati mtu amelala usingizi. Ikitokea wakati mtu yuko macho, wakati mwingine huendana na misisimko ya mwili kabla ya mwako, ikiwa na maana ya kumfanya mtu awe makini na kitu chochote kinachotarajia kutokea. Ndiyo maana baadhi ya watu utakuta wakisema wanaumwa tumbo, kifua au kichwa cha ghafla katika kipindi ambacho taswira ya tukio fulani inakuwa ikitokea akilini mwao, ikiwaambia waende mahali fulani bila kukosa kwa mfano, na kadhalika. Hakuna mtu anaweza kufanya jakamoyo imtokee. Hutokea yenyewe muda wowote kuleta ujumbe, kuhusiana na matukio ya wakati ujao. Kamwe usipuuze wito wa moyo wako.”

“The candle is the light of life that is constantly thriving to hang on and light up the darkness of life. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere was a candle in the wind. He was a fighter fighting the odds to survive. And he did so with incredible power to change the world. Whether your life is long or short upon the earth, it is remarkable that our little flames burns on in spite of the wind, or the challenges of life.”

“Watu wanaohatarisha maisha yao kwa kudharau sheria wakati mwingine hawatakiwi kudharauliwa. Ni sawa na mtu aliyepoteza kila kitu katika maisha yake. Wana uwezo wa kufanya chochote. Serikali ya Meksiko ilipokataa kukidhi matakwa ya El Tigre ya kubadili katiba ya nchi – kuondoa kipengele cha mkataba wa kubadilishana watuhumiwa na washtakiwa – ili akikamatwa asipelekwe Marekani ambako atafungwa na kufia gerezani, El Tigre aliilaani Serikali ya Meksiko. Kujibu mapigo, ya laana ya maluuni, Serikali ya Meksiko ikawakabidhi makamanda 7 wa Kolonia Santita kwa mamlaka za Marekani, na kuongeza juhudi za kumsaka El Tigre mpaka nje ya Amerika ya Kusini na Kaskazini. El Tigre, kuikomoa serikali na kuwalipia kisasi makamanda wote waliouwawa na kufungwa na shirikisho, akamuua Mwanasheria Mkuu wa Serikali (PGR) na maafisa 7 wa Jeshi la Polisi la Nchi (PJF) kulinganisha idadi ya makamanda wake waliopelekwa Marekani – halafu 'akapotea', kabisa; baada ya kutangaza vita na Serikali ya Meksiko!”

“Maisha tunayoishi ni mafupi, maisha ya mbinguni ni ya milele. Fundisha familia yako upendo na hofu ya Mungu, kwani hiyo ndiyo akili kushinda zote. Hekima ya kutunza familia inapatikana katika kitabu cha Mithali cha Agano la Kale.”

“Ikiwa huna pesa na una mke na watoto kwa mfano, mke wako (wanawake walio wengi) hatakuona wa maana kwa sababu ya ustawi wa maisha ya familia yake. Ikiwa una mwanamke asiyekuwa na busara au hekima ya kutosha, au mwanamke ambaye akili zake zimefyatuka kidogo, atakusaliti kutafuta bwana au mtu mwenye maana. Kama huna pesa huna maana kwa mwanamke.”

“Kama ulikuwa ukimwambia mwanao kuwa atakuwa jambazi labda kwa sababu ya fujo zake alipokuwa mdogo, mambo mengi atakayokuwa anayafikiria au anayaota atakapopevuka akili ni ya kihalifu. Kwani hayo ndiyo mambo ya kwanza kabisa kujirekodi katika ubongo wake alipokuwa hajitambui. Lakini kama ulikuwa ukimwambia kuwa atakuwa daktari au mwanasheria, mambo mengi atakayokuwa anayafikiria au anayaota ni ya kidaktari au kisheria. Kuna uwezekano mkubwa akawa daktari au mwanasheria baadaye katika maisha yake.”

“Kuwepo kwa Mti wa Uzima wa Milele katika Bustani ya Edeni (pamoja) na Mti wa Maarifa ya Mema na Mabaya inamaanisha, Adamu na Hawa walikuwa hai kiroho mpaka walipokula tunda la mti wa katikati ambapo hali yao ya maisha ilibadilika. Adamu na Hawa walikufa lakini hawakufa – walikufa baadaye kabisa. Hii inamaanisha kwamba (haya ni mawazo yangu tu) mtu anapokufa anakuwa amekula tunda la mti wa katikati, litakalomwezesha kuendelea kuishi katika hali nyingine ya maisha ambayo sisi hatuijui.”

“Kitu cha kwanza kufanyika mwanadamu anapozaliwa ni kuvuta pumzi ya kwanza katika mapafu ya mwili wake. Cha mwisho kufanyika kabla ya kufa ni kutoa pumzi ya mwisho katika mapafu ya mwili wake. Pumzi iliyoingia kwanza baada ya kuzaliwa, itakuwa ya mwisho kutoka kabla ya kufa. Pumzi ni bora kuliko muda halafu pumzi ni uhai. Bila uhai watu hawataweza kusherehekea mwaka mpya au kufanya chochote. Likumbuke jina la Mwenyezi Mungu katika kila pumzi unayoingiza na kutoa.”

“Kiongozi wa kanda ya Afrika ya Kusini ya Tume ya Dunia Kamishna Profesa Justin Mafuru, alijitolea maisha yake kufanya vitu viwili vya msingi kwa ajili ya dunia: Kukomesha madawa haramu ya kulevya nchini Tanzania na duniani kwa jumla, kupitia Tume ya Dunia, na kutafuta kupitia maabara za CERN ('Conseil Européen pour la Recherche Nucléaire') chembe ndogo ya 'higgs' ('Higgs Boson') inayosemekana kuhusika na uzito ('mass') wa chembe ndogo kumi na sita za atomu kasoro chembe ya mwanga; iliyopotea mara tu baada ya mlipuko wa ulimwengu wa 'Big Bang', miaka bilioni kumi na tatu nukta saba iliyopita kwa faida ya uanadamu.”

“Kipo kitu kinaendelea kufanyika katika siku zetu za furaha na katika siku zetu za huzuni kwa kila mmojawetu hapa duniani bila ya upendeleo wowote. Kitu hicho ni kuingia na kutoka kwa pumzi, au kupumua. Ukiithamini pumzi inayoingia na kutoka ndani ya mwili wako utapata zawadi ya amani katika maisha yako. Utapata pia zawadi ya furaha, uelewa na ufasaha! Ijapokuwa una matatizo mengi katika maisha, kitu bora cha kufanya ni kushukuru Mungu kwa maana wewe ni mzima.”

“Mungu akikubariki kipaji chako watu watasema ni laana. Maisha yako ni sawa na mto. Unakoelekea ni baharini. Lakini sasa umefika kwenye mlango wa bahari. Unahangaika upite wapi kufika baharini, ambapo utaogelea kwa kadiri utakavyoweza. Utakapofika baharini, watu, badala ya kusema umebarikiwa, watasema umelaaniwa, badala ya kukuita malaika, watakuita shetani. Mafanikio hayapimwi kwa pesa au mali kiasi gani unayo, mafanikio yanapimwa kwa amani ya moyo au maisha ya watu kiasi gani umeboresha.”

“Kwa nini mtoto mchanga anapokuwa ananyonya ziwa la mama yake, mara nyingi humwangalia mama yake machoni? Kwa sababu, licha ya macho kuonekana kitu cha ajabu kwake, mtoto mchanga, bila kujitambua, hutamani sana mama yake amwambie neno zuri atakalolitumia baadaye katika maisha yake atakapokuwa mkubwa. Maneno huumba. Ukimwambia mwanao kuwa anaonekana atakuwa jambazi, anaweza kuwa jambazi kweli atakapokuwa mkubwa; ukimwambia kuwa anaonekana atakuwa mwanasheria, anaweza kuwa mwanasheria kweli atakapokuwa mkubwa.”

“Kamera ina athari kubwa sana katika maisha yetu. Inaweza kuharibu taswira ya mtu mbele ya jamii, na inaweza kuharibu maisha ya mtu hali kadhalika. Wasanii wakubwa duniani hawatoki ndani bila ya kuwa nadhifu au bila ya kujipodoa. Kwa nini? Kwa sababu ya wasanii wao wa vipodozi. Wasanii wao wa vipodozi hawataki waajiri wao wawe na taswira mbaya mbele ya wateja wao ambayo ni jamii. Kuwa na taswira mbaya mbele ya jamii kunaweza kusababisha wao (wasanii wa vipodozi) pamoja na waajiri wao, wasiishi vizuri hapa duniani kama wanavyotaka. Kioo ni kitu au mtu. Kama huna uwezo wa kumiliki vipodozi, miliki kioo. Kama huna uwezo wa kumiliki kioo, miliki rafiki. Kioo (hasa kitu) hakina unafiki. Usitoke ndani bila kuridhika na taswira yako.”

“Kumwamini Mwenyezi Mungu wakati wa raha ni rahisi kuliko kumwamini Mwenyezi Mungu wakati wa shida, na utahitaji imani kuendelea kumwamini wakati wa dhiki. Vipindi vigumu katika maisha yetu hutokea kwa kila mmoja wetu. Kuamini ya kwamba Mungu ana makusudi ya lazima kukuondolea vikwazo katika maisha yako ni vigumu sana wakati mwingine, lakini imani ndicho kitu cha muhimu zaidi unachotakiwa kuwa nacho katika kipindi hiki ambacho dunia imekata tamaa. Amani ya Mungu, ambayo huzidi hekima na maarifa yote ya kibinadamu, ni kuliamini neno la Mungu kwamba ni la kweli. Bila imani hutaweza kumfurahisha Mungu. Imani ni ufunguo wa nguvu, uwezo na neema ambavyo Mungu ametupangia. Kwa ufupi, Mungu ni mkubwa kuliko wewe na matatizo yako.”

“Tafuta kitu cha kufanya katika maisha yako unachokiamini zaidi kuliko pesa, kutoa sauti kwa ajili ya watu wasioweza kusikika kwa mfano, na ukishakipata kuwa kiongozi na mkarimu kwa wengine. Kutoa sauti kwa ajili ya watu wasioweza kusikika inaweza kuwa ndiyo nafasi yako uliyopangiwa na Mungu uitumie kwa manufaa ya wengine, si kwa manufaa yako, nafasi za wengine zitatumika kwa manufaa yako. Kuna vitu vingi ambavyo mtu anaweza kufanya; chagua kimoja kinacholeta maana zaidi katika maisha yako na ukifanye hicho, kwa nguvu zako zote.”

“Katika dunia ya leo ambapo mamilioni ya watu hutegemea utandawazi kupata pesa, kuwa na imani kwamba kupokea pesa kutoka kwa mtu usiyemjua au mtu mwenye nia mbaya na wewe ni kikwazo kikubwa cha maendeleo kwa sababu, karibu kila mtu unayekutana naye ni Shetani. Shetani ni mtu yoyote mwenye nia mbaya na wewe. Hivyo, kama uliwahi kuambiwa kwamba kupokea pesa kutoka kwa mtu usiyemjua ni kitu kibaya futa imani hiyo. Utaachaje kupokea pesa kutoka kwa mtu usiyemjua wakati kila siku unamwomba Mungu akusaidie, na Mungu hutenda kazi zake pale tunapojisahau? La sivyo hutapata pesa unayotamani kupata katika maisha yako, na kamwe hutawaamini watu. Zaka huondoa laana ya mapato. Toa zaka kununua pepo uliyopewa na Mungu.”

“Mwili wako una uwezo wa kujua kabla yako kitakachotokea baadaye. Kama una njaa kwa mfano, mwili wako utakwambia. Kama una kiu, mwili wako utakwambia. Kama unaumwa, mwili wako utakwambia. Kama kuna kitu kibaya kinatarajia kutokea katika maisha yako au katika maisha ya mtu mwingine, mwili wako utakwambia. Kuwa makini na alamu zinazotoka ndani ya mwili wako, kwani hizo ni ishara za Roho Mtakatifu kukuepusha na matatizo ya dunia hii.”