Quotessence
Home / Authors / Enock Maregesi

Enock Maregesi Quotes

Author

Filter quotes by topic

Famous Enock Maregesi Quotes

“Mungu ni baba yetu wa kiroho. Hivyo basi, tunajua ya kuwa upendo wake umehifadhiwa ndani ya mioyo yetu. Kwa hiyo, kila mtu ana upendo wa ‘agape’ kwa kiasi fulani; lakini si upendo kamili. Upendo wa ‘agape’ kati ya binadamu na binadamu unahusiana na upendo wa kujitolea kwa ajili ya binadamu wengine. Kila mtu ana kiasi fulani cha upendo huo. Mtu akitaka awe na upendo kamili wa ‘agape’ sharti awe mtiifu na mnyenyekevu mbele za Mungu, na mbele ya binadamu wenzake, sharti ampende Mungu, na sharti ampende jirani yake kama anavyoipenda nafsi yake mwenyewe.”

“Sabato ilianzishwa na Mungu siku ya saba ya uumbaji wake. Siku ya Sabato ni siku takatifu, iliyoko katika Amri Kumi za Mungu, ambayo hatuna budi kuitunza na kuiheshimu. Sheria ya Siku ya Sabato haikufa baada ya kifo cha Yesu Kristo msalabani kama Wakolosai wanavyodai. Wakolosai walifuata falsafa za kipagani, na walizileta falsafa hizo ndani ya mwili wa Kristo ambalo ni kanisa. ‘Usiiamini’ Wakolosai 2:17. Iamini Wakolosai 2:20-23, ambapo Paulo anafundisha Mataifa jinsi ya kuitunza Sabato, na 1 Wakorintho 12:27 ambayo inatoa maana halisi ya Wakolosai 2:17. ‘Mwili wako ni wa Kristo’ ni tofauti na ‘mwili wa Kristo’ na ni tofauti na kanisa. Ukiamini kama mwili wako ni wa Kristo na ni kanisa, utaitunza Sabato.”

“Watoto wadogo wanakufa. Watu wazima wasiokuwa na hatia wanakufa vitani na katika majanga mengine ya asili. Kwa nini? Watoto wadogo wanaokufa walikuja duniani kufanya nini? Kwa nini watu wasiokuwa na hatia wanakufa ilhali Mungu yupo na asiwaepushe na matatizo ya dunia hii? Kama aliweza kuzuia binadamu wasiishi majini kwa sababu watakufa kwa nini asizuie matatizo yasiwapate watoto na watu wazima wasiokuwa na hatia? Sisi ni wadogo sana na Mungu ni mkubwa mno. Jibu hatutaweza kulielewa pamoja na kwamba tumepewa. Hata hivyo, Mungu hababaishwi na mwili. Anababaishwa na roho.”

“Unaweza kuwa umeomba kuhusu jambo fulani kwa muda mrefu bila majibu, lakini siku moja ghafla ukajibiwa wakati umejisahau. Kwa nini? Kwa sababu Mungu hufanya kazi zake kwa siri. Ukiomba jambo kutoka kwa Mungu, huku ukiwa huna kinyongo na mtu yeyote na bila moyo wako kusita wakati ukiomba, tambua katika moyo wako kwamba tayari umeshajibiwa. Kisha lipotezee, hilo jambo, kila siku, usiwe unalikumbukakumbuka, hadi Mungu mwenyewe atakapokujibu. Hata Yesu atakaporudi kila mtu atakuwa amejisahau.”

“Kumwamini Mwenyezi Mungu wakati wa raha ni rahisi kuliko kumwamini Mwenyezi Mungu wakati wa shida, na utahitaji imani kuendelea kumwamini wakati wa dhiki. Vipindi vigumu katika maisha yetu hutokea kwa kila mmoja wetu. Kuamini ya kwamba Mungu ana makusudi ya lazima kukuondolea vikwazo katika maisha yako ni vigumu sana wakati mwingine, lakini imani ndicho kitu cha muhimu zaidi unachotakiwa kuwa nacho katika kipindi hiki ambacho dunia imekata tamaa. Amani ya Mungu, ambayo huzidi hekima na maarifa yote ya kibinadamu, ni kuliamini neno la Mungu kwamba ni la kweli. Bila imani hutaweza kumfurahisha Mungu. Imani ni ufunguo wa nguvu, uwezo na neema ambavyo Mungu ametupangia. Kwa ufupi, Mungu ni mkubwa kuliko wewe na matatizo yako.”

“Yusufu alikuwa hohehahe kabla na baada ya kuuzwa na nduguze kama mtumwa nchini Misri. Hakuwa na pesa, hakuwa na elimu, hakujuana na viongozi wa serikali. Lakini kwa vile alikuwa na Mungu, Mungu alimbariki mpaka watu wote wakashangaa. Yusufu alikuwa maskini ili mimi na wewe tuwe na tumaini leo, kwamba tukiwa na Mungu katika maisha yetu hatutatafuta utajiri. Utajiri ndiyo utakaotutafuta sisi.”

“Mungu anapokupa kipaji anategemea ukitumie vizuri kwa ajili ya wengine. Usipokitumia vizuri kwa ajili ya wengine, ama kwa uvivu au kwa woga, atawapa wengine wakitumia kwa ajili yako. Ukitumia vipaji vyako vizuri, Mungu atakuongezea maradufu. Yaani, ukitumia muda wako vizuri atakuongezea muda. Ukitumia nguvu zako vizuri atakuongea nguvu. Ukitumia pesa yako vizuri atakuongezea pesa. Ukitumia ukarimu wako vizuri atakuongezea ukarimu. Ukitumia maarifa yako vizuri atakuongezea maarifa.”

“Tafuta kitu cha kufanya katika maisha yako unachokiamini zaidi kuliko pesa, kutoa sauti kwa ajili ya watu wasioweza kusikika kwa mfano, na ukishakipata kuwa kiongozi na mkarimu kwa wengine. Kutoa sauti kwa ajili ya watu wasioweza kusikika inaweza kuwa ndiyo nafasi yako uliyopangiwa na Mungu uitumie kwa manufaa ya wengine, si kwa manufaa yako, nafasi za wengine zitatumika kwa manufaa yako. Kuna vitu vingi ambavyo mtu anaweza kufanya; chagua kimoja kinacholeta maana zaidi katika maisha yako na ukifanye hicho, kwa nguvu zako zote.”

“Mungu anataka tujifunike kwa ngao yake. Yaani, tuwe na imani iliyokomaa katika Bwana na yeye atatufunika. Maana ya kauli hiyo ni kwamba kila kiungo cha miili yetu kuanzia unyayo hadi kichwa lazima kifunikwe kwa silaha ya Mungu, ambayo Mungu anaiita panoplia. Panoplia haimo katika kamusi ya Kiswahili au Kiingereza, lakini maana yake ni ‘ngao kamili ya Mungu’. Hii si tu silaha ya Mungu. Ni silaha kamili ya Mungu tunayotakiwa kujifunika kwayo.”

“Ukiwa makini, nadhani, utapata maana ya ujumbe unaopewa na Roho Mtakatifu kwa wale wanaomwamini Mungu au ‘daemon’ (tofauti na ‘demon’) kwa wale wasiomwamini Mungu. Mimi, kwa mfano, huwa najali muda. Jicho langu likicheza au kiungo changu chochote cha mwili kikiuma ghafla na kuacha, au hata kisipoacha, jambo lolote ninalolifikiria muda huo ambapo jicho linacheza au kiungo changu cha mwili kinauma najua ni ujumbe kutoka kwa Mungu na una uhusiano na jambo hilo ninaloliwaza. Hivyo, kuanzia sekunde hiyo napaswa kuwa makini sana na jambo lolote ninalolifikiria.”

“Katika dunia ya leo ambapo mamilioni ya watu hutegemea utandawazi kupata pesa, kuwa na imani kwamba kupokea pesa kutoka kwa mtu usiyemjua au mtu mwenye nia mbaya na wewe ni kikwazo kikubwa cha maendeleo kwa sababu, karibu kila mtu unayekutana naye ni Shetani. Shetani ni mtu yoyote mwenye nia mbaya na wewe. Hivyo, kama uliwahi kuambiwa kwamba kupokea pesa kutoka kwa mtu usiyemjua ni kitu kibaya futa imani hiyo. Utaachaje kupokea pesa kutoka kwa mtu usiyemjua wakati kila siku unamwomba Mungu akusaidie, na Mungu hutenda kazi zake pale tunapojisahau? La sivyo hutapata pesa unayotamani kupata katika maisha yako, na kamwe hutawaamini watu. Zaka huondoa laana ya mapato. Toa zaka kununua pepo uliyopewa na Mungu.”

“Soma sana. Andika sana. Ongea na watu kuhusu mambo ya muhimu unayoyafikiria. Tumia intaneti na maktaba kwa makini kwa ajili ya utafiti, kwa sababu habari nyingi za intaneti na maktaba haziaminiki. Kama una wazo kichwani mwako lizungumze kwa watu kama mazungumzo ya kawaida, ili upate maoni yao ya dhati, bila kusahau kuandika kwa siri wazo lolote jipya utakalolipata kutokana na mazungumzo hayo. Maana Mungu anaweza kuwasiliana na mtu mwingine yeyote yule akupe wazo, litakaloongeza maana zaidi katika mawazo ambayo tayari unayo.”