Quotessence
Home / Authors / Enock Maregesi

Enock Maregesi Quotes

Author

Filter quotes by topic

Famous Enock Maregesi Quotes

“Kuna siri ambayo wanaume hawaijui kuhusu wanawake. Wanawake wenye umri wa miaka kumi na nane hadi ishirini na mbili wana mapenzi ya kweli. Ishirini na mbili hadi ishirini na nne wana mawenge. Ishirini na nne hadi ishirini na saba wanajitambua. Ishirini na saba hadi thelathini wana hofu na mashaka mengi. Thelathini hadi thelathini na tano wana msongo wa mawazo. Thelathini na tano hadi arobaini na mbili ndoa nyingi huvunjika. Kwa hiyo, kuwa makini na wanawake na wanaume hasa wanawake na wanaume wa kundi la sita. Wanawake na wanaume hasa wanawake na wanaume wa kundi la sita, wengi wao wana DNA ya wapenzi wao wa zamani.”

“Nini kingetokea kama Adamu na Hawa wasingekula tunda la Mti wa Maarifa ya Mema na Mabaya mpaka siku ya Sabato? Mungu angewaruhusu kula na lengo la uumbaji wa Mungu lingekamilika. Wanadamu wakifuata Amri Kumi za Mungu katika maisha yao watakuwa na uwezo maalumu ambao baadaye utawawezesha, kupitia Roho Mtakatifu, kuwa na maarifa ya siri ya uumbaji wa Mungu.”

“Lakini kuna ndoto takatifu na kuna ndoto za kishetani. Ndoto takatifu hutokea wakati akili imetulia baada ya mwili wote kupumzika, kama ambavyo usiku unavyokuwa kimya na kila kitu kimetulia, karibu na saa za alfajiri, ambapo mfumo wa usagaji chakula unakuwa umemaliza kazi yake. Kipindi hicho malaika wa Mungu hutufunulia siri kuhusu ulimwengu huu, ili kwamba tutakapoamka asubuhi tuwe na baadhi ya maarifa yaliyojificha ndani ya maandiko ya vitabu vitakatifu; kwa sababu malaika wa Mungu ndiye anayetawala ufahamu wetu, kama ambavyo Mungu anavyotawala hiari yetu, na kama ambavyo nyota zinavyotawala miili yetu. Lakini kwa wale waliokomaa kiimani malaika mwema anaweza kuwafunulia siri wakati wowote, haijalishi wamelala au wameamka. Kwa ajili ya ujanja wa Shetani ndiyo maana Mungu hutufunulia siri zake, ili tujihadhari naye.”

“Falaki maana yake ni kundi la nyota na sayari ikiwemo dunia. Falaki yetu inaitwa Njiamaziwa, ‘the Milky Way galaxy’, yenye mabilioni ya mifumo ya jua ukiwemo wa kwetu. Mungu alisimamisha jua katika falaki ya Njiamaziwa kwa ajili ya Yoshua, ili apate muda wa kutosha kuwashinda maadui zake – wanajeshi wa mataifa matano. Kila mtu alishangaa sana kipindi hicho. Kila mtu anashangaa sana kipindi hiki. Mungu akikubariki watu watasema wewe ni mchawi. Hawatajua nini kilitokea. Kwani kwa Mungu hakuna kinachoshindikana. Mungu aliweza kutenda miujiza kwa ajili ya Yoshua, na kwa ajili ya wana wa Israeli huko Gibeoni na huko Aiyaloni, anaweza kutenda miujiza kwa ajili yako popote pale ulipo. Mungu anachotaka kutoka kwako ni imani ya kweli juu yake, kwa mwili na kwa roho yako yote.”

“Kuna vitu vitatu ndani ya mtu: kuna hiari, kuna ufahamu, na kuna mwili. Hiari inatawaliwa na Mungu; ufahamu unatawaliwa na malaika mwema; mwili unatawaliwa na nyota lakini chini ya usimamizi wa malaika wema: malaika wema walisimamisha jua na mwezi kwa ajili ya Yoshua na wana wa Israeli juu ya Gibeoni na katika bonde la Aiyaloni, walirudisha jua nyuma kwa ajili ya Hezekia mfalme wa Yuda na kwa ajili ya nabii Isaya, na waliifanya dunia ‘kuvaa koti’ ghafla wakati wa kusulubiwa kwa Mwanakondoo wa Mungu Anayeondoa Dhambi. Moyoni ni mahali patakatifu. Hata malaika wema hawawezi kuona ndani ya moyo wa mtu, ni Mungu pekee mwenye uwezo wa kufanya hivyo, na alichokihifadhi Mungu ndani ya moyo huo ni hiari ya mtu ya kuchagua mema au mabaya.”

“Usiingilie mambo ya mtu mwingine bila kibali kutoka kwa Mungu. Kuingilia mambo ya mtu mwingine bila kibali kutoka kwa Mungu ni dhambi. Dhambi hiyo itakuathiri. Hivyo, jali mambo yako – ya mwingine Mungu anayafanyia kazi – hadi utakapoitwa na Mungu kuingilia kati. Kuingilia kati mambo ya mtu mwingine kunaweza kuathiri mpango wa Mungu katika maisha yake. Hivyo, acha.”

“Wewe kuingilia mambo ya John ni sawa na kusema, ‘Mungu umeshindwa hebu ngoja na mimi nijaribu; ngoja niingilie kati kukusaidia juu ya maisha ya John Doe.’ Hiyo ni dhambi. Tena ni dhambi kubwa. Unajifananisha na Mungu; kwamba Mungu wa John Doe ameshindwa kwa hiyo mungu wewe ndiye utakayemtatulia matatizo yake. Amri kuu ya kwanza ya Mungu inasema, ‘Usiwe na miungu mingine ila mimi.’ Kuingilia mambo ya John tayari umevunja amri ya kwanza ya Mungu kwa kujifanya Mungu. Mungu ana mpango na maisha ya John, na anatumia matatizo yake kumfikisha kwenye takdiri aliyompangia. Hivyo, wewe si Mungu, acha Mungu afanye kazi yake. Mungu akikuruhusu kuingilia kati, yaani John akiamua kwa hiari yake mwenyewe kukuomba msaada wa mawazo au ushauri, maana yake ni kwamba Mungu amekuchagua wewe kuwa sehemu ya mafanikio ya John Doe.”

“Inavyoonekana, kadiri mtu anavyozidi kupata elimu ndivyo anavyozidi kudharau uwepo wa Shetani na uwepo wa Mungu pia. Lakini, kwa upande mwingine, ndivyo anavyoonekana hajasoma sana na ndivyo Shetani anavyozidi kulaumiwa kwa kila dhambi inayotendeka. Kuna elimu ya kidunia na kuna elimu ya kidini. Huwezi kutawala dunia bila elimu ya kidunia, kwa sababu Shetani anajua ukiipata elimu hiyo hutajua kama yupo; na huwezi kutawala dunia bila elimu ya kidini, kwa sababu Mungu anajua ukiipata elimu hiyo utajua kama yupo. Hivyo, utamdharau Mungu ukipata elimu ya kidunia, utamheshimu Mungu ukipata elimu ya kidini.”

“Siku ya kwanza dhambi ya kwanza ilipotendwa Mungu alitoa kafara ya kwanza ya wanyama kwa ajili ya wazazi wetu wa kwanza Adamu na Hawa. Adamu na Hawa walikuwa uchi, baada ya kutenda dhambi, Mungu akawalaani lakini akawapa uwezo wa muda mfupi wa kutubu dhambi zao ili awasamehe! Kutokana na ngozi za wanyama hao walipata mavazi na kutokana na damu ya wanyama hao walipata fursa ya kuishi na kutubu dhambi zote walizozitenda. Bila hivyo wasingepata muda wa kusamehewa.”

“Kama damu haina maana kwa nini Mungu anaipenda? Kama damu haina maana kwa nini Shetani anaipenda? Mungu ni roho, Shetani ni roho, lakini damu ni kitu kinachoonekana kwa macho. Kwa nini damu ni kitu cha muhimu kiasi hicho kwa Mungu na kwa Shetani pia? Damu ni pato la ziada la ufunuo wa kiroho. Yaani, damu ni sehemu ya ulimwengu wa roho. Mungu ndiye aliyetengeneza damu kwa malengo anayoyajua yeye mwenyewe, hata Shetani hajui kwa asilimia mia umuhimu wa damu katika ulimwengu unaoonekana na katika ulimwengu usioonekana. Damu ina uwezo wa kuzuia mapepo kutoka kuzimu yasiharibu mipango ya maisha ya watu na ina uwezo wa kuondoa dhambi. Kafara ya damu inapotolewa inaimarisha uhusiano kati ya mtu na ulimwengu wa roho. Roho unayoitolea kafara inasikiliza shida zako papo hapo na kila unachoomba aghlabu kinatekelezwa. Ukitoa kafara kwa ajili ya Shetani, Shetani atasikiliza shida zako. Ukitoa kafara kwa ajili ya Mungu, Mungu atasikiliza shida zako. Tatizo kubwa la mwanadamu ni dhambi! Jibu la tatizo hilo ni damu ya Yesu Kristo.”

“Mungu alimuumba mwanadamu ili aitawale dunia. Shetani tayari alikuwepo wakati Adamu anaumbwa. Adamu na Hawa walipokula tunda la mti wa katikati, walikufa kiroho – Yaani, walipoteza sura na asili ya Mungu – Shetani akawashinda kuanzia kipindi hicho na kuendelea. Tulizaliwa katika dhambi. Kila mtu anayezaliwa anazaliwa katika dhambi. Njia pekee ya kuikomboa sura na asili ya Mungu ni kumpokea Yesu (Kristo) kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako.”

“Kuna vita za aina mbili zinazopiganwa hapa duniani: vita ya maisha na vita ya dhambi. Unaweza kushinda vita ya maisha (maisha ya raha) lakini ukashindwa vita ya dhambi (maisha ya laana). Kushinda vita ya dhambi ni lazima umkaribishe Mwana wa Mungu Mfalme wa Amani, Yesu Kristo wa Nazareti Aliye Hai, kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako.”

“Vita ya dhambi hupiganwa katika uwanja wa akili na katika uwanja wa mwili kati ya Shetani na Mungu. Hutumia silaha kuu ya uongo na silaha kuu ya ukweli. Mungu anataka tuujue ukweli. Shetani anataka tuujue uongo. Kushinda vita ya dhambi huna budi kutumia neno la Mungu, kama Yesu alivyolitumia kumshinda Shetani wakati akijaribiwa katika Mlima wa Majaribu wa Jangwa la Yuda.”

“Wenye dhambi watafufuliwa na wataungana na Ibilisi kuipiga Yerusalemu Mpya itakayokuwa inang'inia hewani, huku Yesu na watakatifu wote wakiwa hawana silaha yoyote; lakini vilevile wakiwa hawapigwi kwa silaha yoyote. Shetani atakapoonekana kushindwa, Yesu atawasha ‘kibiriti cha kiroho’. Mafuta yote yaliyopo ardhini dunia nzima yatalipuka na kugeuza ardhi yote kuwa ziwa la moto, na hivyo wenye dhambi wote kupata aibu ya milele.”

“Mfalme Sulemani alikuwa mtu mwenye hekima kuliko wote ulimwenguni. Anatushauri, “Adui yako akiwa ana njaa, mpe chakula; Tena akiwa ana kiu, mpe maji ya kunywa; Maana utatia makaa ya moto kichwani pake; Na BWANA atakupa thawabu (Mithali 25:21-22). Yesu anasema jambo fulani linalofanana sana na hilo katika mafundisho Yake yaliyofuata (Mathayo 5:44-45). Kitendo cha kutukanwa, kupigwa, kushtakiwa au kulazimishwa kubeba mzigo mzito usio wa kwako kinaweza kusababisha mafutu mabaya kabisa katika asili ya binadamu. Yaani, chuki, hasira, ukatili na hata vurugu. Lakini pale wale waliobarikiwa kuwa na hekima wanapojikuta katika majaribu makubwa kama hayo tabia yao haitakiwi kuwa ya shari, inda au ya kulipiza kisasi. Bali inatakiwa kuwa ya kusaidia, kuwa na ridhaa ya kutenda mambo mema, na kuwa mwema kwa wengine siku zote.”

“Msamaha si jambo dogo. Watu wadogo, watu wenye uwezo mdogo wa kufikiri, hawawezi kupambana na changamoto za msamaha. Msamaha ni kwa ajili ya watu wenye macho kama ya tai wanaoweza kuona mbali ambao wako tayari kushindwa vita ili washinde vita. Hewa inaingia ndani ya mapafu na kutoka; chakula kinaingia ndani ya mwili na kutoka; mwanamasumbwi anapigana bila kugombana; injini ya gari haiwezi kusukuma gari mbele au nyuma bila kutoa hewa katika paipu ya ekzosi. Lakini kile kinachoingia moyoni mwako hakitoki! Maumivu yanapoingia ndani ya moyo yanapaswa kutoka nje kama yalivyoingia kwa sababu, yasipotoka yatatengeneza sumu ndani ya moyo wako na yatatengeneza sumu ndani ya roho yako pia. Sumu hiyo itahatarisha safari yako ya mbinguni na Mungu hatakusamehe tena. Badala ya yule aliyekukosea kuumia, utaumia wewe uliyekosewa. Yesu anaposema samehe saba mara sabini hatanii. Usiposamehe, hutasamehewa.”

“Wananchi wanapokosa huduma za muhimu za kijamii (kama vile afya, elimu, chakula, malazi, na ulinzi) ilhali wanalipa kodi, na wameajiri serikali kuwaendeshea nchi kwa kiapo cha uaminifu wa vitabu vitakatifu, watakosa imani na serikali yao! Vilevile wataathirika kiuchumi, kijamii na kisiasa, na vita itaweza kutokea kati ya wananchi na serikali, au wananchi kwa wananchi wataweza hata kujidhuru wenyewe – nikimaanisha vita ya wenyewe kwa wenyewe. Serikali ikifuata maadili ya kazi, na kuacha udikteta na urasimu wa aina yoyote ile, au ikifanya kazi kulingana na misingi ya katiba ya nchi; wananchi watapata huduma za kijamii kama wanavyostahili, na ndoto ya haki na ustawi wa jamii itaweza kutimia. Hata hivyo, serikali inaweza kuwadhulumu wananchi wake kwa sababu ya usalama wao.”

“My novels are set in a global space and pace. However, I have never visited most of the places. I wrote my first book in London but the story took the reader to places in Mexico, Denmark and Russia, and carefully avoided London. I access these global locations with my feet planted in front of my computer. I will use my internet connection to carefully enter the streets of a foreign city and find out how long it will take my main character to get from the airport to the city center – and if there are any shortcuts on the way. I wanted to do something new. The world is becoming a global village and we have to understand these different cultures. There is a Danish culture, an Israeli culture and so on. So if you want to go to Denmark, then read the book.”

“Watu wakikuonyesha tabia zao za ndani kabisa usisubiri wakuonyeshe tena ndiyo uwaamini. Waamini kwa mara ya kwanza. Mtu, kwa mfano, akionyesha kwa mara ya kwanza kuwa si mwaminifu mwamini. Anajijua zaidi kuliko unavyomjua. Aidha, mtu akikwambia anakupenda halafu akakupiga ni mnafiki. Maneno yake yatasema anakupenda, vitendo vyake vitasema hakupendi. Ukiwa makini na matendo ya mtu, si maneno yake, utamjua. Sikiliza maoni ya watu! Kuwa makini na matendo ya mtu.”

“Mapenzi, kama ilivyo kwa vitu vyote hapa ulimwenguni, hayawezi kuwepo bila kujumuishwa na fizikia na kemia yake! Bila kemia hakuna mapenzi ya kudumu. Tamaa ya ngono kimsingi huanza pindi unapokutana na mtu. Tamaa hiyo huweza kukua na kuwa kitu kingine kadiri muda unavyokwenda lakini chanzo kinakuwepo toka siku ya kwanza mlipokutana. Kemikali inayosababisha tamaa ya ngono na hata kuikuza tamaa hiyo ni 'phenyl ethylamine' ('fino itholamine') au PEA ambayo ni kemikali ya mapenzi ndani ya ubongo. Husisimua watu na huongeza nguvu za kimwili (fizikia) na kihisia (kemia). Tamaa husababisha mtu azalishe PEA nyingi zaidi, kitu kinachosababisha kujisikia kizunguzungu (cha hisia za kimapenzi) na dalili zingine kama magoti kutetemeka, jasho kutoka viganjani na kutokutulia. Kemikali hii inapozalishwa kwa kiwango kikubwa, hutuma alamu ('signals') kutoka kwenye ubongo mpaka kwenye viungo vingine vya mwili na kutumika kama 'dopamine' au 'amphetamine' ambazo ni kemikali za ulevi ndani ya ubongo. Iwapo unajiuliza kwa nini wewe au mtu mwingine unavutiwa na mtu ambaye hamwendani kimapenzi, inaweza kuwa ni kwa sababu una kiwango kikubwa cha kemikali hizo kuliko mwenzako, kitu ambacho huzidi uwezo wa kutumia kichwa na kutoa maamuzi bora kulingana na akili ya kuzaliwa. Kwa jumla, mapenzi yote ya kweli uhitaji angalau kiwango kidogo cha PEA kwa wale wanaopendana. Cha msingi kukumbuka ni kwamba kemikali hizi huja kwa vituo, nikiwa simaanishi kwamba tamaa ya ngono hupotea pale mtu anapoelekea kwenye uhusiano wa kudumu. Lakini mambo hubadilika. Hatuwezi kuvumilia zile hisia kali kadiri tunavyozidi kusafiri kuelekea kwenye uhusiano wa kudumu na kwenye maisha ya pamoja yenye furaha. Katika uhusiano wenye afya hata hivyo matatizo hutokea hapa na pale. Chanzo cha Murphy na Debbie kupendana kilikuwa kemia zaidi kuliko fizikia. Kama hakuna kemia hakuna mapenzi.”

“Aidha, tunaweza kupata inkishafi kutokana na asili ya miili yetu, matukio fulani ya wakati ujao yana asili yake katika ndoto za binadamu. Ndoto hizo au maono hayo ni ishara ya kile kinachokuja mbele katika maisha ya mtu; kama vile afya, ugonjwa au hatari. Ukiota kuhusu moto, hiyo ni ishara ya hasira – unatakiwa kuwa na hekima; ukiota kuhusu mimba na unajifungua, hiyo ni ishara ya kuwa katika mchakato wa kutengeneza wazo jipya – unatakiwa kushukuru; ukiota unaruka angani, hiyo ni ishara ya tumaini – unatakiwa kushukuru; ukiota kuhusu maji au kiowevu kingine chochote kile, hiyo ni ishara ya siri na wakati mwingine ni ishara ya kuwa na matatizo ya kiafya kama utaota kuhusu maji machafu – unatakiwa kuwa msiri na msafi; ukiota kuhusu ardhi, hiyo ni ishara ya huzuni – unatakiwa kuomba; na ukiota kuhusu Yesu, hiyo ni ishara ya mafanikio – unatakiwa kushukuru.”

“Lengo kuu la Kolonia Santita kuuza madawa hayo ni kuwafadhili askari wa msituni wa Kolombia (magorila wa vyama visivyokuwa rasmi vya kisiasa au vyama haramu vya kisiasa) kushika hatamu za uongozi wa Kolombia, kwa makubaliano ya Kolonia Santita kutawala biashara ya kokeini ya taifa hilo la Amerika ya Kusini. WODEA lazima ilizuie Shirika la Madawa ya Kulevya la Kolonia Santita kuuza madawa hayo kwa gharama yoyote ile, pesa au damu, kutetea afya na amani ya dunia.”