Quotessence
Home / Authors / Enock Maregesi

Enock Maregesi Quotes

Author

Filter quotes by topic

Famous Enock Maregesi Quotes

“Mpelelezi wa Tume ya Dunia kutoka Israeli Daniel Yehuda Ben-Asher Ebenezer, Mhebrania aliyeishi Givat Ram, Jerusalem, na mke wake mrembo Hadara na mtoto wake mzuri Navah Ebenezer, alikuwa Ukanda wa Gaza siku alipopigiwa simu na Kiongozi wa Kanda ya Asia-Australia ya Tume ya Dunia U Nanda – kutoka Copenhagen kuhusiana na wito wa haraka wa kuonana na Rais wa Tume ya Dunia. Yehuda aliondoka usiku kwenda Yangon, Myama, ambapo alionana na U Nanda na kupewa maelekezo yote ya kikazi aliyotakiwa kuyafuata. Mbali na maelekezo yote ya kikazi aliyotakiwa kuyafuata, Nanda alimkabidhi Yehuda kachero wa Kolonia Santita Mandi Dickson Santana (bila kujua kama Mandi ni kachero wa Kolonia Santita) ili amsindikize mpaka stendi ya mabasi ya Maubin, nje ya Yangon. Baada ya hapo Yehuda alisafiri mpaka Copenhagen ambapo yeye na wenzake walikabidhiwa Operation Devil Cross, ya kung’oa mizizi ya Kolonia Santita duniani kote. Yehuda alifanya kosa kubwa kuonana na kachero wa Kolonia Santita Mandi Santana! Kwa sababu hiyo, sauti na picha ya Yehuda vilichukuliwa, watu wengi walikufa katika miji ya Copenhagen na Mexico City.”

“Kumwamini Mwenyezi Mungu wakati wa raha ni rahisi kuliko kumwamini Mwenyezi Mungu wakati wa shida, na utahitaji imani kuendelea kumwamini wakati wa dhiki. Vipindi vigumu katika maisha yetu hutokea kwa kila mmoja wetu. Kuamini ya kwamba Mungu ana makusudi ya lazima kukuondolea vikwazo katika maisha yako ni vigumu sana wakati mwingine, lakini imani ndicho kitu cha muhimu zaidi unachotakiwa kuwa nacho katika kipindi hiki ambacho dunia imekata tamaa. Amani ya Mungu, ambayo huzidi hekima na maarifa yote ya kibinadamu, ni kuliamini neno la Mungu kwamba ni la kweli. Bila imani hutaweza kumfurahisha Mungu. Imani ni ufunguo wa nguvu, uwezo na neema ambavyo Mungu ametupangia. Kwa ufupi, Mungu ni mkubwa kuliko wewe na matatizo yako.”

“Kwa mfano, uko kwenye mashindano ya mbio za mita 100. Utakapofika kwenye kamba, mwisho wa hizo mita 100, utakuwa umechoka sana. Lakini kocha anakuhimiza uendelee mbele mita nyingine 50! Unaweza kufika ukiwa mzima au unaweza kufika ukiwa umezimia. Lakini usijali. Ukiendelea mita nyingine 50 utakuwa umetumia uwezo wako wote uliopewa na Mwenyezi Mungu. Ukitumia kanuni hiyo katika maisha yako ya kawaida utaweza kufanikiwa.”

“Mpenzi. Sikiliza. Magaidi yaliyomuua Marciano yana mtandao dunia nzima na watu wote wanayajua. Yanaitwa Kolonia Santita. Tatizo hata hivyo ni moja: Hakuna mtu amewahi kuthibitisha au kutoa ushuhuda wa uhalifu wao ili watiwe nguvuni. Huendesha maisha yao kibabe na yana kila mbinu ya kukwepa sheria, ndani na nje ya Meksiko. Watu wengi wameuwawa kwa sababu ya Kolonia Santita. Ukileta kidomodomo yanakuua; au yanakupa notisi ya kuhama mji au nchi, ukakae mbali na Meksiko au Mexico City.”

“Majambazi huwapenda wanaowapenda. Chukulia mfano huu: Mimi na Wanda ni marafiki, OK? Baba yake, au genge la baba yake, hataweza kunidhuru au kuwadhuru watu ninaowapenda kwa sababu tu ya urafiki na mtoto wake. Na yeye anaweza kufumbiwa macho akifanya makosa kwa sababu mimi na mtoto wake ni marafiki wakubwa. Murphy, hapa Meksiko tuna kitu kinaitwa Bima ya Utekaji Nyara ('Ransom Insurance'). Zamani nilikuwa nalipa dola milioni kumi za Marekani kama bima ya utekaji nyara; Lisa alikuwa analipa milioni nne na Wanda bado analipa milioni mbili mpaka sasa hivi. Baada ya mimi na Lisa kujenga urafiki na Wanda, malipo yetu ya bima yamepungua mpaka dola milioni moja kwa mwaka.”

“Kesho yake Ijumaa Rais wa Meksiko alirudi kutoka Panama na aliomba kuonana na Vijana wa Tume; alitaka kuwapongeza binafsi, na kuwapa nishani za heshima kwa mchango wao mkubwa kwa Jamii ya Meksiko. Randall Ortega alilipeleka ombi hilo kwa Rais wa Tume ya Dunia; Rais wa Tume ya Dunia akakaa na Kamati ya Usalama ya Tume ya Dunia na kumrudishia Randall Ortega jawabu, kwamba Vijana wa Tume waliruhusiwa kuonana na Rais wa Meksiko na baadhi ya maafisa wa juu wa serikali ya shirikisho. Saa mbili usiku wa siku hiyo, Ijumaa, kulifanyika sherehe ndogo ya siri nyumbani kwao Debbie; sherehe iliyohudhuriwa na Rais wa Meksiko na mke wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Meksiko, Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya Nchini Marekani, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu Nchini Meksiko, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, maafisa wa tume na watu wengine wa muhimu katika kazi ya Vijana wa Tume.”

“Kilometa mbili na ushei kidogo kutoka katika sanamu la Yesu Mtoto liitwalo Niñopa, katika Kanisa la Parokia ya Manispaa ya Xochimilco ('Sochimiliko') la Iglesia de San Bernardino de Siena, Mexico City, kulikuwa na nyumba ndogo ya siri ('safe house') ya Kolonia Santita iliyojengwa bila uzio wa ukuta au seng’enge isipokuwa miti iliyopandwa kuizunguka bila mpangilio wowote. Ndani ya nyumba hiyo Mpelelezi Maarufu Duniani John Murphy alikuwa akiteswa na magaidi kumi na mbili; waliokuwa wakiendelea kushangaa jinsi alivyookoka katika ajali ya ndege iliyoua watu zaidi ya mia tatu huko Uholanzi, na jinsi alivyoweza kuingia katika ofisi ya siri ya Panthera Tigrisi, kitu kilichomchanganya akili Tigrisi na makompade wote wa Kolonia Santita duniani kote. Bila Mtoto wa Rais wa Meksiko Debbie Patrocinio Abrego, na mwanasesere wa nyoka wa Mtoto wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Lisa Madrazo Graciano, John Murphy angeanguka.”

“Ngumi ya Ambilikile ilitua barabara katika kichwa cha Brookshield na kuleta madhara makubwa. Sehemu moja ya kichwa, cha Brookshield, ilibonyea kabisa! Kimya kilichotawala kiliwasisimua mashabiki. Walipovamia ulingo, kushuhudia kisichoweza kufikirika, walitoka pale wakiwa na hakika ya asilimia 100; kwamba John alikuwa na nyundo (au chuma chochote) katika mfuko wake wa bukta – aliyoitoa (harakaharaka), wakidhani ni mtindo wa kipigo, na kumpondea mwenzake kichwani! Ile haikuwa nyundo. Wala haukuwa uchawi. Ilikuwa ngumi, imara, ya uzito wa kilo 90; uzito wote wa John Ambilikile.”

“Afrika isomeshe watu wake, na itumie vizuri mapato yanayotokana na mauzo ya rasilimali zake kwa faida ya jumla ya wananchi wa nchi zake, kusudi baadaye wawe wataalamu wa rasilimali za nchi zao wenyewe, kuepukana na utumwa wa rasilimali. Rasilimali za Afrika zina miiko na masharti yake.”

“Sina jinsi. Nguzo ya maisha yangu ni historia ya maisha yangu. Historia ya maisha yangu ni urithi wa watu waliojifunza kusema hapana kwa ndiyo nyingi – waliojitolea vitu vingi katika maisha yao kunifikisha hapa nilipo leo – walionifundisha falsafa ya kushindwa si hiari. Siri ya mafanikio yangu ni kujitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu wote. Hiyo wote katika herufi kubwa. Wote katika herufi kubwa (WOTE) si neno la kawaida falau katika nukuu hii ya mafanikio. Linamaanisha kujitahidi kwa kadiri ya uwezo wako wote uliopewa na Mwenyezi Mungu. Watu wengi hujitahidi kwa kadiri ya uwezo wao. Usijitahidi kwa kadiri ya uwezo wako. Jitahidi kwa kadiri ya uwezo wako WOTE.”

“Hakimu na Kuhani Mkuu wa Shilo Eli alipata matatizo makubwa wakati wa mgogoro wa Waisraeli na Wafilisti, kati ya mwaka 2871 na 2870 Kabla ya Kristo. Mara tu baada ya kupewa taarifa ya kifo cha watoto wake wawili, Hofni na Finehasi, na kutwaliwa kwa Sanduku la Agano la Bwana wa Majeshi lililohifadhi Amri Kumi za Mungu, Eli alianguka kutoka katika kiti chake na kufariki papo hapo akiwa na umri wa miaka 98. Aidha, mkwe wa Eli, mke wa Finehasi, alijifungua ghafla na kufariki alipopata taarifa ya kifo cha mkwewe na taarifa ya kuuwawa kwa mumewe na ya kutekwa nyara kwa Sanduku la Agano. Mwanajeshi kutoka Benyamini falaula angetumia hekima na busara kutoa taarifa ya kifo na ya kutwaliwa kwa Sanduku la Agano huenda Eli asingefariki, na huenda mkwewe asingejifungua mtoto njiti na huenda asingekufa siku hiyo. Kwani Sanduku la Agano lilirejeshwa nchini Israeli, na Wafilisti wenyewe, baada ya miezi saba tangu litwaliwe, na kifo cha watoto wa Eli yalikuwa mapenzi ya Mungu. Hivyo Eli asingeweza kuzuia kifo cha watoto wake, na Wafilisti wasingeweza kukaa na Sanduku la Agano milele. Lakini katika kafara ya Isaka ambapo Isaka aliamua kujitoa kafara mwenyewe kumfurahisha Mungu na baba yake kama Yesu alivyoamua kujitoa kafara mwenyewe kumfurahisha Mungu na baba yake wa mbinguni, Sara angekufa kama Ibrahimu hangetumia hekima alipomwambia anakwenda kumtolea Bwana kafara ya mwanakondoo wakati akijua anakwenda kumtoa Isaka mtoto wa pekee wa Sara. Hekima inatoka moyoni, busara inatoka mdomoni. Kwa vile suala la kutoa taarifa mbaya kwa mtu ni gumu kwa yule anayetoa na kwa yule anayepokea, hekima na busara havina budi kutumika.”

“Kiingereza kililetwa na wakoloni wa Kiingereza kutoka Uingereza na walikitumia katika masuala yote ya kiutawala ya Afrika Mashariki. Kililetwa pia na wamisionari waliojenga shule na kuwafundisha Kiingereza wanafunzi na walimu na watu wengine wa kawaida, kwa lengo la kuwasaidia katika kazi yao ya kueneza dini kama wakalimani, hivyo kufanya Kiingereza kienee zaidi kuliko Kiswahili.”

“Yusufu alikuwa hohehahe kabla na baada ya kuuzwa na nduguze kama mtumwa nchini Misri. Hakuwa na pesa, hakuwa na elimu, hakujuana na viongozi wa serikali. Lakini kwa vile alikuwa na Mungu, Mungu alimbariki mpaka watu wote wakashangaa. Yusufu alikuwa maskini ili mimi na wewe tuwe na tumaini leo, kwamba tukiwa na Mungu katika maisha yetu hatutatafuta utajiri. Utajiri ndiyo utakaotutafuta sisi.”

“Pesa itolewe kwa masharti au bila masharti chukua, kwani huyo aliyeitoa si yake. Benki, kwa mfano, ikitaka kukupa mkopo itakuwa na masharti yake; chukua, iwapo utakubaliana na masharti hayo. Jambazi akikupa pesa ili ukafanyie ujambazi chukua pia. Lakini hiyo usiipeleke kanisani, ipeleke serikalini. Serikali itajua jinsi ya kupambana na huyo aliyekupa hiyo pesa, na hiyo pesa itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama nchini. Pesa kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama nchini ni sawa na zaka, au sadaka, na wewe utabarikiwa kwa kupata nyingine.”

“Mungu anapokupa kipaji anategemea ukitumie vizuri kwa ajili ya wengine. Usipokitumia vizuri kwa ajili ya wengine, ama kwa uvivu au kwa woga, atawapa wengine wakitumia kwa ajili yako. Ukitumia vipaji vyako vizuri, Mungu atakuongezea maradufu. Yaani, ukitumia muda wako vizuri atakuongezea muda. Ukitumia nguvu zako vizuri atakuongea nguvu. Ukitumia pesa yako vizuri atakuongezea pesa. Ukitumia ukarimu wako vizuri atakuongezea ukarimu. Ukitumia maarifa yako vizuri atakuongezea maarifa.”