Quotessence
Home / Authors / Enock Maregesi

Enock Maregesi Quotes

Author

Filter quotes by topic

Famous Enock Maregesi Quotes

“Siku ya kwanza dhambi ya kwanza ilipotendwa Mungu alitoa kafara ya kwanza ya wanyama kwa ajili ya wazazi wetu wa kwanza Adamu na Hawa. Adamu na Hawa walikuwa uchi, baada ya kutenda dhambi, Mungu akawalaani lakini akawapa uwezo wa muda mfupi wa kutubu dhambi zao ili awasamehe! Kutokana na ngozi za wanyama hao walipata mavazi na kutokana na damu ya wanyama hao walipata fursa ya kuishi na kutubu dhambi zote walizozitenda. Bila hivyo wasingepata muda wa kusamehewa.”

“Kama damu haina maana kwa nini Mungu anaipenda? Kama damu haina maana kwa nini Shetani anaipenda? Mungu ni roho, Shetani ni roho, lakini damu ni kitu kinachoonekana kwa macho. Kwa nini damu ni kitu cha muhimu kiasi hicho kwa Mungu na kwa Shetani pia? Damu ni pato la ziada la ufunuo wa kiroho. Yaani, damu ni sehemu ya ulimwengu wa roho. Mungu ndiye aliyetengeneza damu kwa malengo anayoyajua yeye mwenyewe, hata Shetani hajui kwa asilimia mia umuhimu wa damu katika ulimwengu unaoonekana na katika ulimwengu usioonekana. Damu ina uwezo wa kuzuia mapepo kutoka kuzimu yasiharibu mipango ya maisha ya watu na ina uwezo wa kuondoa dhambi. Kafara ya damu inapotolewa inaimarisha uhusiano kati ya mtu na ulimwengu wa roho. Roho unayoitolea kafara inasikiliza shida zako papo hapo na kila unachoomba aghlabu kinatekelezwa. Ukitoa kafara kwa ajili ya Shetani, Shetani atasikiliza shida zako. Ukitoa kafara kwa ajili ya Mungu, Mungu atasikiliza shida zako. Tatizo kubwa la mwanadamu ni dhambi! Jibu la tatizo hilo ni damu ya Yesu Kristo.”

“Mungu alimuumba mwanadamu ili aitawale dunia. Shetani tayari alikuwepo wakati Adamu anaumbwa. Adamu na Hawa walipokula tunda la mti wa katikati, walikufa kiroho – Yaani, walipoteza sura na asili ya Mungu – Shetani akawashinda kuanzia kipindi hicho na kuendelea. Tulizaliwa katika dhambi. Kila mtu anayezaliwa anazaliwa katika dhambi. Njia pekee ya kuikomboa sura na asili ya Mungu ni kumpokea Yesu (Kristo) kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako.”

“Kuna vita za aina mbili zinazopiganwa hapa duniani: vita ya maisha na vita ya dhambi. Unaweza kushinda vita ya maisha (maisha ya raha) lakini ukashindwa vita ya dhambi (maisha ya laana). Kushinda vita ya dhambi ni lazima umkaribishe Mwana wa Mungu Mfalme wa Amani, Yesu Kristo wa Nazareti Aliye Hai, kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako.”

“Vita ya dhambi hupiganwa katika uwanja wa akili na katika uwanja wa mwili kati ya Shetani na Mungu. Hutumia silaha kuu ya uongo na silaha kuu ya ukweli. Mungu anataka tuujue ukweli. Shetani anataka tuujue uongo. Kushinda vita ya dhambi huna budi kutumia neno la Mungu, kama Yesu alivyolitumia kumshinda Shetani wakati akijaribiwa katika Mlima wa Majaribu wa Jangwa la Yuda.”

“Msamaha si jambo dogo. Watu wadogo, watu wenye uwezo mdogo wa kufikiri, hawawezi kupambana na changamoto za msamaha. Msamaha ni kwa ajili ya watu wenye macho kama ya tai wanaoweza kuona mbali ambao wako tayari kushindwa vita ili washinde vita. Hewa inaingia ndani ya mapafu na kutoka; chakula kinaingia ndani ya mwili na kutoka; mwanamasumbwi anapigana bila kugombana; injini ya gari haiwezi kusukuma gari mbele au nyuma bila kutoa hewa katika paipu ya ekzosi. Lakini kile kinachoingia moyoni mwako hakitoki! Maumivu yanapoingia ndani ya moyo yanapaswa kutoka nje kama yalivyoingia kwa sababu, yasipotoka yatatengeneza sumu ndani ya moyo wako na yatatengeneza sumu ndani ya roho yako pia. Sumu hiyo itahatarisha safari yako ya mbinguni na Mungu hatakusamehe tena. Badala ya yule aliyekukosea kuumia, utaumia wewe uliyekosewa. Yesu anaposema samehe saba mara sabini hatanii. Usiposamehe, hutasamehewa.”

“Maumivu ya matatizo ya yule aliyekukosea hayana tofauti na maumivu ya matatizo ya wewe uliyekosewa. Adui yako (kwa mfano) akifiwa na mke aliyempenda sana, atajisikia vibaya kama utakavyojisikia vibaya kufiwa na mke uliyempenda sana. Kuwa na huruma kwa waliokukosea, wakati wa shida.”

“Damu, mto wa maisha unaotiririsha maji yake mwilini kwa kusukumwa na pampu za moyo na kuchujwa na fizi za mapafu, inaundwa na seli na maji yaitwayo utegili au maji ya damu, ambayo kazi yake ni kusafirisha oksijeni na virutubisho katika kila sehemu ya mwili, ndani yake kuna roho. Mungu alitoa kafara ya damu kwa ajili ya Adamu na Hawa katika Bustani ya Edeni. Ibrahimu alitoa kafara ya damu kwa ajili ya Israeli ijapokuwa mapenzi ya Mungu kwa Israeli yalikwisha baada ya kusulubiwa kwa Yesu Kristo. Wana wa Israeli walitoa kafara za damu kwa ajili ya wokovu wa watoto wao wa kwanza na watoto wa kwanza wa wanyama wao nchini Misri. Mungu alitoa kafara ya damu ya Yesu Kristo nchini Israeli kwa ajili ya wanadamu wote duniani. Damu ya mwanakondoo ina nguvu kuliko maombi, imetiwa wakfu na Mwenyezi Mungu na ina uhusiano mkubwa na ulimwengu wa roho. Ukifunikwa na damu ya mwanakondoo Shetani hatakuona. Shetani asipokuona, utafanikiwa.”

“Maana halisi ya falsafa ya 'Nitakuwa tayari kufungwa kwa ajili ya matatizo ya watu', au Falsafa ya Kufungwa, ni uvutano mkubwa uliopo kati ya Roho Mtakatifu na Roho wa Shetani kwa sisi wanadamu wote. Jambo lolote baya limtokealo mwanadamu husababishwa na Shetani na si Mungu na watu hupata matatizo kwa sababu ya kudharau miito ya mioyo yao wenyewe, au kudharau kile Roho Mtakatifu anachowambia. Unaweza kuvunja sheria kwa manufaa ya wengi kwani mibaraka haikosi maadui. Ukifungwa kwa kuvunja sheria kwa ajili ya manufaa ya wengi watu watakulaani lakini Mungu atakubariki. Kwa nguvu ya uwezo wa Roho Mtakatifu Mungu atamshinda Shetani kwa niaba yako. Tukijifunza namna ya kuwasiliana na Roho Mtakatifu hatutapata matatizo kwani Mungu anataka tuishi kwa amani katika siku zote alizotupangia, licha ya damu yetu kuwa chafu. Mtu anapokufa kwa mfano, Roho wa Shetani amemshinda Roho Mtakatifu na Roho Mtakatifu hatalipendi hilo kwa niaba ya Mungu. Ikitokea mtu akayashinda majaribu ya Shetani katika kipindi ambacho watu wote wameyashindwa; mtu huyo amebarikiwa na Mungu, ili aitumie mibaraka hiyo kuwaepusha wenzake na roho mbaya wa Shetani. Nikisema 'Kwa nguvu ya uwezo wa Roho Mtakatifu Mungu atamshinda Shetani kwa niaba yako' namaanisha, Roho Mtakatifu ana uwezo wake na Roho wa Shetani ana uwezo wake pia. Ukimshinda Roho wa Shetani uwezo wa Roho Mtakatifu umekuwa mkubwa kuliko uwezo wa Roho wa Shetani, na ukishindwa kumtii Roho Mtakatifu uwezo wa Roho wa Shetani umekuwa mkubwa kuliko uwezo wa Roho Mtakatifu, ilhali uwezo wa Mungu ni mkubwa kuliko wa Roho Mtakatifu na wa Roho wa Shetani kwa pamoja. Mungu humtumia Roho Mtakatifu kumlindia watoto wake ambao ni sisi dhidi ya Shetani … Kila akifanyacho Roho Mtakatifu hapa duniani ni kwa niaba ya Mungu, na tukimtii Roho Mtakatifu Mungu atamshinda Shetani kwa niaba yetu. Mtu anapofungwa kwa kutetea maslahi ya umma wewe unayemfunga umemtii Roho wa Shetani. Yule anayefungwa amemtii Roho Mtakatifu maana amebarikiwa, na mibaraka haikosi maadui.”

“Ukifuata kanuni ya nguvu ya uvutano uhitaji kujua jinsi utakavyofanikiwa. Kazi yako ni kuwaza tu kwa namna inavyotakiwa. Waza na amini kwa asilimia mia moja. Mengine yote mwachie Mungu au ulimwengu. Mungu pekee ndiye anayekupa njia na bahati, ili wewe ufanikiwe. Atakupa nguvu ya kufanya kazi na ujanja wowote utakaohitajika, katika harakati hizo za mafanikio yako.”

“Sigara zilizidi kuvutwa, ndani ya nyumba, na magaidi wale wawili, wakati Murphy akisinzia kudanganyia kama kweli nguvu zilishamwisha. Alimfikiria tena mpenzi wake Sophia, safari hii sana. Alimkumbuka Debbie; hakujua alikuwa wapi na hakujua mama yake angefanya nini kama Debbie angekufa, na Murphy ndiye aliyetoka naye. Debbie alimuuma zaidi. Alimkataza kufa kwa ajili ya mchumba wake. Sasa alikufa kwa ajili ya mtu ambaye hakumjua. Murphy alijilaumu kumtongoza na kumchukua kwao na kulala naye na kula chakula chake cha kifalme. Wazazi wake wangejisikiaje kama angekufa, tena katika mazingira ya kutatanisha kama yale. Kufa alijua angekufa; lakini Mungu angemsaidia, awaage watu wake.”

“Yesu alikuwa binadamu ili afe kama binadamu kwa ajili ya binadamu. Alikufa msalabani ili sisi wote tuokoke. Lakini Shetani hataki hilo litokee. Akiingilia uumbaji wa Mungu toka tumboni mwa binadamu, binadamu atakayezaliwa hatakuwa na uwezo wa kuongoka. Atakuwa na roho ya jini itakayomjua Shetani badala ya kumjua Mungu. Hivyo kurudi kwa Yesu kwa mara ya pili hakutakuwa na maana, kwa sababu hakutakuwepo na mtu wa kuokolewa.”

“Maamuzi ya Adamu na Hawa ya kutokumtii Mungu juu ya Mti wa Maarifa ya Mema na Mabaya, ndiyo yaliyosababisha Yesu Kristo ajitolee maisha yake ili wengine waweze kuishi. Hakuna Mungu bila Yesu. Mtafute Yesu, kukomboa sura na asili ya Mungu.”

“Kila mmoja wetu ana kitu cha kutoa. Wengine wana pesa, wengine wana vipaji, wengine wana muda. Vipaji vyote tulivyopewa na Mungu, vikubwa au vidogo, hatuna budi kuvitumia kiukarimu kwa watu wanaovihitaji. Tunapofanya hivyo tunaleta mabadiliko katika dunia kwa ajili ya watu fulani, na tunapata maana halisi ya maisha na toshelezo la moyo katika maisha yetu.”

“Wakati mwingine inaweza kuonekana kuwa kadiri unavyozidi kujitolea kwa ajili ya watu wengine ndivyo unavyozidi kuwa maskini, lakini hii si kweli. Huduma kwa ajili ya watu wengine huleta maana fulani na ukamilifu katika maisha yetu kwa namna ambayo utajiri, madaraka na mali haviwezi kushindana nao. Mungu hababaishwi na kiasi gani unatoa. Anababaishwa na imani uliyonayo wakati unatoa. Ukitoa kidogo inatosha. Ukitoa kingi inatosha pia.”

“Siri ya mafanikio yako ni chumba chako. Dali linasema anga ndicho kipimo cha kufikiria; Dirisha linasema utazame nje uone fursa zilizopo ulimwenguni; Feni linasema uwe mtulivu usikurupuke kufanya lolote; Kalenda inasema uwe mtu anayekwenda na wakati; Kioo kinasema ujitazame na ujiamini kabla ya kutenda lolote; Kitabu cha dini kinasema unapaswa kumwamini Mungu ili uishi; Kitanda kinasema ujifunze kuwa na likizo; Mlango unasema usipitwe na fursa ya aina yoyote ile hapa duniani; Saa inasema kila sekunde ina thamani sana katika maisha yako hivyo tumia muda wako vizuri. Amka uishi.”

“Dunia huzunguka kwenye mhimili wake na huzunguka jua. Jua huzunguka kwenye mhimili wake na huzunguka falaki. Dunia hutumia takriban siku moja kuzunguka kwenye mhimili wake, na hutumia takriban mwaka mmoja kuzunguka jua. Jua hutumia takriban siku ishirini na tano kuzunguka kwenye mhimili wake, na hutumia takriban miaka milioni mia mbili na hamsini kuzunguka falaki. Yoshua alisimamisha jua ili lisizunguke kwenye mhimili wake na lisizunguke falaki. Kwa sababu jua lilisimama, kila kitu kilichoathiriwa na jua hilo kilisimama pia ikiwemo dunia. Hata hivyo, kwa sababu tukio la Yoshua kusimamisha jua na mwezi yalikuwa maajabu kutoka kwa malaika wema, malaika wema ndiyo wanaojua kwa hakika nini kilitokea. Yoshua alikuwa sahihi kusema jua lisimame si dunia isimame. Mungu aliweza kusimamisha jua kwa ajili ya Yoshua kuwashinda maadui zake, kwa sababu aliamini. Mungu anaweza kusimamisha jua kwa ajili yako kuwashinda maadui zako, ukiamini. Mungu anapokuwa na wewe matatizo yako yako matatizoni.”

“Binti yako mwenye umri wa miaka kumi na nne kwa mfano, anaomba umnunulie gari kama ulivyofanya kwa kaka yake mwenye umri wa miaka kumi na nane. Mara ya kwanza unamwambia utamnunulia atakapofikisha umri wa miaka kumi na nane kama ulivyofanya kwa kaka yake. Lakini baada ya wiki moja binti yako anakuomba tena kitu kilekile, yaani gari. Utajisikiaje? Utakereka, sivyo? Jinsi utakavyokereka binti yako kukuomba kitu ambacho tayari ameshakuomba, ndivyo Mungu anavyokereka sisi kumwomba vitu ambavyo tayari tumeshamwomba. Ukiomba kitu kwa mara ya kwanza Mungu amekusikia, tayari ameshaandaa malaika wa kukuletea jibu. Unachotakiwa kufanya, baada ya kuomba, shukuru mpaka jibu lako litakapofika. Mungu huthamini zaidi maombi ya kushukuru kuliko maombi ya kuomba. Binti yako anachotakiwa kufanya baada ya kukuomba gari ni kukushukuru mpaka gari yake itakapofika, si kukuomba mpaka gari yake itakapofika.”

“Ningependa kujitokeza leo kutoa salamu zangu za rambirambi kwa Watu wa Musoma; kutokana na ajali mbaya ya mabasi ya J4 Express, Mwanza Coach, na gari ndogo aina Nissan Terrano, iliyotokea Ijumaa tarehe 5/9/2014 katika eneo la Sabasaba mjini Musoma. Kulingana na vyombo vya habari, watu 39 wamefariki dunia. Wengine wengi wamejeruhiwa vibaya. Mali za mamilioni ya fedha zimeteketea kabisa. Hii ni ajali mbaya na ya kusikitisha mno kwa maana halisi ya maneno mabaya na ya kusikitisha. Maneno hayataweza kuelezea kikamilifu huzuni niliyonayo juu ya ajali hii ya kutisha, lakini Mungu awasaidie wale wote waliofiwa au walioguswa na ajali hiyo kwa namna yoyote ile, na awasamehe marehemu wote dhambi zao na awapumzishe mahali pema peponi. Wale wote waliofariki hawataweza kurudi huku, lakini sisi tutakwenda huko.”

“Shetani na wafuasi wake wako kifungoni sasa hivi kwa sababu dhambi walizotenda hazisameheki. Dhambi ya kumkana Mungu na kumkubali Shetani haisameheki. Kwa maana nyingine, ukimuuzia Shetani roho yako jina lako halitaandikwa katika kitabu cha uzima litaandikwa katika kitabu cha mauti. Ukibidika kuuza roho, usimuuzie Shetani, muuzie Yesu.”

“Bibi Martha Maregesi aliishi maisha mazuri sana hapa duniani. Alibarikiwa na Mungu. Aliishi miaka 84 – siku 30660 badala ya siku 25550 tulizopangiwa na Mungu. Katika uhai wake wote, kwa wale wote aliowalea, hakuna mtoto wake hata mmoja aliyefariki kabla yake. Hakuna mjukuu wake hata mmoja aliyefariki kabla yake. Hakuna kitukuu chake hata kimoja kilichofariki kabla yake. Bibi yangu ametimiza mwaka mmoja kamili leo hii, tangu amefariki dunia Novemba 4 mwaka 2014 mjini Musoma. Tunamkumbuka leo akiwa amefariki kama tulivyomkumbuka jana akiwa hai. Nguvu ya sala zetu imfanye Mwenyezi Mungu aendelee kumsamehe dhambi zake zote, na amweke mahali anapostahili, Amina.”

“Mungu ni mtakatifu na kwa maana hiyo hatendi dhambi. Hivyo, hauwi wala hatesi. Tunajiua na kujitesa wenyewe. Ametupa hiari ya kuchagua mema au mabaya. Lakini anamtumia Shetani kama wakala wake wa kutoa adhabu kwa binadamu pale tunapoenenda sawasawa na machukizo yake. Damu ina nguvu kuliko Shetani na ina nguvu kuliko kuzimu. Unapojifunika kwa damu ya Mwanakondoo, Shetani hataweza kukuona. Hivyo, hataweza kukudhuru. Lakini usipojifunika kwa damu ya Mwanakondoo, Shetani atakuona. Hivyo, atakudhuru. Atakudhuru kwa sababu Mungu atakuwa ameruhusu akudhuru, kwa sababu ya uhuru wa kuchagua mema au mabaya aliotupatia, ijapokuwa ana uwezo wa kuzuia asikudhuru. Kwa mtindo huo Mungu anakuwa ametoa adhabu kwa binadamu.”

“Kama miaka 1000 ya duniani ni sawa na siku moja ya Mungu; hivyo basi, miaka 930 aliyoishi Adamu ni sawa na siku 0.93 au saa 22:32 za Mungu. Kwa hiyo, ili siku ya Mungu itimie Adamu alipaswa kuishi miaka 70 (siku 0.07 au saa 1:68) zaidi! Ukiidadavua saa 1:68 unapata saa 2:08. Kulingana na muda wa mbinguni tunapaswa kuishi kwa muda wa saa 2:08! Muda huo ni mfupi sana.”

“Tunazaliwa, kuteseka na kufa kwa sababu ya dhambi ya asili ya wazazi wetu wa kwanza (Adamu na Hawa). Kama Hawa asingekubali kudanganywa na Shetani, tungezaliwa bila uchungu, tungeishi bila kuteseka na tusingekufa milele. Lakini haya ndiyo mawazo yangu: Mungu Ahusiki na dhambi, Ahusiki na mwili, Anahusika na roho. Hivyo, mtu anapofariki mwili unabaki duniani lakini roho inarudi kwa Mungu; kwani Yeye ndiye aliyeitengeneza na kuiweka katika moyo wa mtu. Mimi na wewe ni viumbe vyenye thamani kubwa sana mbele za Mwenyezi Mungu; mapenzi Yake kwetu hayana masharti yoyote. Hainiingii akilini (hata kidogo) kumtesa mtu unayempenda kiasi hicho milele, wakati uwezo wa kumwokoa unao.”

“Mpinga Kristo atakapoona imeshindikana kuwanyamazisha, Eliya na Enock, huku akitamba kwamba yeye ndiye Yesu Kristo ambaye kila mtu ndiye aliyekuwa akimsubiri arudi kwa mara ya pili; na kwamba yeye anatoka katika ukoo wa mfalme Daudi, ili watu waamini kama kweli yeye ndiye Yesu Kristo, ataamuru Eliya na Enock wauwawe hadharani kama wahubiri wengine. Eliya na Enock watakapouwawa, Mungu atawafufua na watarudi mbinguni wakiwa wameonja mauti kama binadamu mwingine yeyote yule. Hapo mlango wa rehema utakuwa umefungwa. Muda wowote kuanzia hapo Yesu atarudi, kwa mara ya pili, na kwa ajili ya ufufuo wa kwanza.”

“Damu ya Mwanakondoo ina nguvu kuliko maombi. Mungu hauwi, Anamtumia Shetani kama wakala wake wa kutoa adhabu kwa binadamu. Ukifunikwa na damu ya Mwanakondoo Shetani, ambaye ni wakala, hatakuona. Lakini Mungu atakuona. Bila kafara ya damu hakuna msamaha wa dhambi. Bila kafara ya damu hakuna mafanikio.”

“Kwa vile taifa la Israeli lilipoteza haki yake ya upendeleo, Mungu aliahidi kuliharibu kama alivyoyaharibu mataifa ya Waamori na Wamisri. Watu wa Israeli walishafika mbali sana kiasi cha Mungu kutokutegemea tena toba kutoka kwao. Kuna muda wa fursa na kuna muda ambao fursa haipo tena. Nafasi ya Israeli ya kutubu ilishafikia mwisho. Kama alivyokuwa amepigana vita vyao kwa ajili yao katika siku za nyuma sasa Mungu alipigana nao. Pamoja na ujasiri na utaalamu wao wote wasingependelewa tena. Mambo ambayo mwanzo yaliipa Israeli nguvu katika vita yaliwageukia.”

“Kuna ndoto za mchana na kuna ndoto za usiku. Ndoto za mchana ni maono ya kile ambacho roho inatamani kuwa. Ndoto za usiku ni maono yanayotokea wakati akili imetulia baada ya mwili wote kupumzika. Ukiota kuhusu moto, hiyo ni ishara ya hasira; ukiota kuhusu maji, hiyo ni ishara ya siri; ukiota kuhusu ardhi, hiyo ni ishara ya huzuni; ukiota kuhusu Yesu, hiyo ni ishara ya mafanikio. Kitu cha kwanza kufanya unapoota ndoto za kishetani, utakapoamka, mwombe Mungu akunusuru kutoka katika matatizo yoyote yanayokunyemelea; au yanayomnyemelea mtu mwingine yoyote yule, hata usiyemjua. Ubongo ni kitu cha ajabu kuliko vyote ulimwenguni na umetengenezwa na Mungu. Ndoto zinapatikana ndani ya ubongo. Ubongo unapatikana ndani ya ufahamu. Ufahamu mtawala wake ni malaika mwema. Malaika mwema anajua siri ya ndoto. Kila mtu anaota na kila ndoto ina maana yake. Rekodi ndoto zako kila siku kwa angalau mwezi mzima kupata maana halisi ya ndoto hizo, na kujua kwa nini ulizaliwa.”

“Shetani hawezi kusoma ndani ya mioyo ya wanadamu mpaka wanadamu wenyewe wamwonyeshe. Ukionyesha tamaa ya ngono, Shetani atakupa ngono. Ukionyesha tamaa ya ulevi, Shetani atakupa ulevi. Ukionyesha tamaa ya wizi, Shetani atakupa wizi. Ukionyesha tamaa ya chuki, Shetani atakupa chuki. Ukionyesha tamaa ya upendo, Mungu atakupa upendo. Kama kuna ubishi kati ya moyo wako na akili yako, fuata moyo wako.”

“Tovuti za miadi (‘dating sites’) hutumia ‘optimal stopping’ kuwachagulia watu wachumba wao. Wanachofanya ni kwamba wanachagua watu 100. Wanaondoa 37% ya kwanza ya wale ambao sifa zao haziendani na sifa unazozitaka. Kisha wanakuchagulia mtu waliyeona ni bora zaidi kuliko wote waliobakia. Huyo waliyekuchagulia anaweza kuwa mke au mume bora. Lakini Mungu ana mipango yake. Unaweza kushangaa mke au mume bora akatoka kwenye 37% ya wale walioachwa.”

“Maombi yako yasipojibiwa usikate tamaa, Mungu alishakusikia na tayari alishaandaa malaika wa kukuletea jibu. Jibu wakati mwingine huchelewa kufika kwa sababu ya nguvu za giza. Usiwe na haraka, muda wako ukifika utajibiwa.”